Rwanda kutoa mikopo ya nyumba kwa watu wa kipato cha chini

Rwanda kutoa mikopo ya nyumba kwa watu wa kipato cha chini

Wananchi wenye kipato cha chini wanaweza kupewa mkopo wa kununua au kujijengea nyumba
Rwanda kutoa mikopo kwa watu zaidi ili wapate nyumba / Photo: AP

Benki ya Maendeleo ya Rwanda (BRD) imefanya mageuzi katika mpango wa nyumba za bei nafuu, ili kuwezesha watu zaidi kumiliki nyumba.

Wananchi sasa wanaweza kupata mkopo wa nyumba kulingana na uwezo wao wa kifedha, ikiwa ni kati ya dola za marekani 4434 na 8500 .

Wanaopata chini ya dola 180, kwa mwezi, wanaweza kupata mikopo ya riba nafuu na kuweza kujipatia nyumba popote nchini.

Wanaweza kuamua kununua nyumba iliyo tayari au kujjijengea, bila kulazimika kungoja zile ambazo wawekezaji wanajenga.

Kumekuwa na changamoto ya wale ambao wana mapato madogo chini ya dola 180 kama walimu kutokuwa na mwanya wa kupata mikopo ya nyumba .

Serikali ya Rwanda inasema kiwango cha dola milioni 150 ambayo ilipewa na benki ya dunia kusaidia mpango wa nyumba za bei nafuu hakitatosha.

Serikali inasema kuna idadi kubwa ya Wanyarwanda wanaohitaji makazi. Takriban asilimia 73 ya fedha zimetumika hadi sasa. Mpango huo ulilenga kusaidia watu 6,000 kuwa wamiliki wa nyumba, huku 4,000 wakiwa tayari wamenufaika.

Sera ya makazi ya gharama nafuu ya Rwanda inasema nyumba ya bei nafuu haipaswi kuzidi dola za Marekani 35,479, na muda wa kulipa mkopo huu unaweza kufika hadi miaka 20.

TRT Afrika na mashirika ya habari