Serikali ya Rwanda inasema inapanga kutoa makazi mapya kwa watu walioathiriwa na mvua kubwa. / Picha wengine.            

Serikali ya Rwanda inasema inapanga kutoa makazi mapya kwa watu walioathiriwa na mvua kubwa katika sehemu tofauti nchini.

Watakaonuafika ni waathiriwa wa tangu Oktoba 2023.

Wilaya 14 zina jamii ya watu ambao wanafaa kuhamishwa haraka iwezekanavyo.

Wilaya hizo ni pamoja na Rubavu, Karongi, Rutsiro, Ngororero, Nyabihu, Burera, Rusizi, Rulindo, Gicumbi, Gakenke, Nyamasheke, Nyamagabe, Musanze, na Muhanga.

Katika mpango huo, nyumba 2,763 zitajengwa upya huku nyumba 1,322 zitakarabatiwa na angalau 342 zitajengwa chini ya awamu ya kwanza.

"Tunaweza kuwahamisha watu kabla ya majanga kutokea na kuwaweka upya katika maeneo salama. Inabidi tushirikiane na Wizara ya Serikali za Mitaa kuwahamisha wale walio katika maeneo hatarishi,” waziri anayesimamia usimamizi wa dharura, Albert Murasira, alisema wakati wa mkutano wa kitaifa.

Ikiwa bado ni msimu wa mvua kubwa, inatabiriwa kuwa watu wengi wataendelea kuathiriwa.

"Tunakumbana na mvua kubwa na tunatarajia mvua kubwa zaidi hata Aprili na Mei. Tunapaswa kujiandaa kwa majanga. Tunafanya kazi na shirika la hali ya hewa la Rwanda, na shirika la anga ili kutambua maeneo yenye hatari kubwa ya watu.

Watu wengine watapewa vipande vya ardhi katika sehemu salama.

Kwa wale ambao nyumba zao ziliharibiwa na mvua hiyo kubwa licha ya kutokuwa katika maeneo yaliyotengwa kuwa ya hatari, serikali imesema bado watapata msaada.

Nyumba zao zilizoharibika zitakarabatiwa.

TRT Afrika