Rwanda imesema kuwa Kituo cha Matibabu cha Rwanda (RBC), mwishoni mwa mwezi huu, kitaanzisha kutoa dawa ya sindano kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi kama njia mojawapo ya kupunguza maambukizi mapya.
Dawa hizo zinazojulikana kama pre-exposure prophylaxis (PrEP), ni aina ya dawa inayotumika kuzuia maambukizi ya Ukimwi.
Hasa, PrEP inahusisha matumizi ya dawa za kurefusha maisha na kuwakinga watu wasio na virusi ili kupunguza hatari ya kuvipata.
Dawa ambayo Rwanda inapanga kuisambaza ni sindano ya muda mrefu ya Cabotegravir (CAB-LA), aina ya PrEP inayofanya kazi kwa muda mrefu kwenye misuli.
Sindano mbili za kwanza hutolewa katika kipindi cha wiki nne, ikifuatiwa na sindano kila baada ya wiki nane.
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilitoa miongozo mipya mwaka 2022 ya matumizi ya CAB-LA kama kinga ya pre-exposure prophylaxis (PrEP) kwa Ukimwi .
Shirika hilo lilihimiza nchi kuzingatia "chaguo hili linalofaa sana kwa watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa Ukimwi."
"Tuliona changamoto kwa kuzingatia PrEP ya aina ya tembe za kumeza, na tunaamini kuwa PrEP ya sindano inaweza kuwa suluhisho," Dkt. Ikuzo alisema. "Tunapanga kuanza kuifanyia majaribio katika vituo viwili vya afya ili kutathmini ikiwa itakubalika na wateja na kubaini kama inaweza kutumika kama suluhu mpya. Ikiwa kiwango cha kukubalika kiko juu, tutaiongeza kote nchini,” aliongeza.
Kwa matumizi ya CAB-LA, watu hutumia dozi moja, mara moja kila baada ya miezi miwili, hii ikiwa afueni kutokana na hitaji la vidonge vya kila siku hadi sindano ya kila miezi miwili.
Dawa hiyo ya sindano inatengenezwa na kampuni ya ViiV Healthcare, kampuni ya kimataifa ya kutengeneza dawa zinazohusiana na Ukimwi, na inamilikiwa na makampuni ya dawa za GSK, ikiwa Pfizer na Shionogi ni wanahisa.
Kampuni inayotengeneza dawa hiyo ViiV Healthcare, imesema zaidi ya dozi milioni mbili za cabotegravir zitapatikana mwaka wa 2025-2026 ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
Februari 2024 Zambia ilianza matumizi ya dawa ya sindano ya kuzuia Ukimwi.