Vita nchini Sudan vimewakosesha makazi zaidi ya watu milioni 11, kulingana na Umoja wa Mataifa. / Picha: AFP

Idadi ya waliouawa katika Al-Hilaliya, mji ulio katikati mwa jimbo la Al Jazirah nchini Sudan, imeongezeka na kufikia zaidi ya 200 kufuatia wiki mbili za mzingiro na mashambulizi yanayoendelea ya kundi la wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF).

RSF iliongeza mashambulizi yake katika jiji hilo kuanzia Oktoba 25, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Muungano wa Madaktari wa Sudan, na idadi hiyo ikiwa ni pamoja na vifo kutokana na ugonjwa, njaa, na mateso.

Muungano huo uliripoti uhaba mkubwa wa huduma za afya kutokana na kuzingirwa huku ikibaini kuwa wakazi wengi wamelazimika kunywa maji yasiyo salama na kusababisha magonjwa ya milipuko.

Gharimu pesa

"Vikosi vya RSF viliwakamata wakazi katika misikiti kadhaa (jijini), na haviwaruhusu kuondoka isipokuwa walipe kiasi kikubwa cha pesa," iliongeza taarifa hiyo.

RSF bado haijajibu madai haya.

Tangu katikati ya Aprili 2023, Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan na RSF vimehusika katika mzozo ambao umesababisha vifo vya zaidi ya 20,000 na kuwakimbia karibu watu milioni 10, kulingana na UN.

Kumekuwa na ongezeko la wito kutoka kwa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa kutaka kumaliza mzozo huo, kwani vita hivyo vimewasukuma mamilioni ya Wasudan kwenye ukingo wa njaa na vifo kutokana na uhaba wa chakula, huku mapigano hayo yakienea katika majimbo 13 kati ya 18 ya Sudan.

TRT Afrika