Mnamo Mei 11, 2023, mpishi Mnigeria Hilda Baci aliwashikilia mashabiki wake kote ulimwenguni alipoanza mbio za marathon za upishi ili kujaribu kuvunja Rekodi ya Dunia ya Guinness kwa muda mrefu zaidi wa kupika na mtu binafsi.
Alifanikiwa baada ya siku nne baadaye wakati aligonga saa 100, ingawa hii ilirekebishwa baadaye na Rekodi ya Dunia ya Guiness kuwa saa 93 na dakika 11.
Wakati wa msururu huo wa mapishi, Baci alipika zaidi ya milo 200 aliyowalisha watu 4,000 waliofika kwenye ukumbi huo. Aliruhusiwa tu kupumzika kwa dakika 5 kila saa.
Hii ilikuwa kazi ya kuchosha, lakini alijiandaa vipi kwa shughuli hii?
Ekemini Ekerette, anayejulikana kwa utani kama Kemem, ni mkufunzi wa kibinafsi wa Hilda ambaye alihusika kumtayarisha kimwili na kiakili kwa changamoto hiyo. Aliiambia TRT Afrika kwamba kulikuwa na mara nyingi timu yake ilihofia kwamba hatafanikiwa.
‘’Kinachofanya hili kuwa la ajabu na muhimu ni kwamba hakuwa mtu mwenye uzoefu wa kufanya mazoezi kila mara katika gym , na kwa hivyo hili lilikuwa geni kwake. Ilitubidi kumfundisha kila kitu— mazoezi ya kukimbia, jinsi ya kufanya mazoezi mbalimbali.’’
Hofu na maumivu
‘’Tulifanya mazoezi mengi ya msingi na ya nguvu ya tumboni, mgongoni na sehemu ya chini ya mwili kama vile mapaja na kiunoni. yalikuwa mazoezi makali. lakini Ilitubidi kujumlisha kwasababu asipojiandaa vyema kimwili na kiakili, huenda asingeweza kudumu muda wote huo.’’
Changamoto hiyo kwa kweli ilikuwa ya kuogofya kwa sababu, ili kutawazwa mmiliki wa rekodi mpya, Hilda alilazimika kuvunja rekodi iliyowekwa na Tondon, mpishi wa Kihindi ambaye alipika kwa saa 87 na dakika 45 bila kukoma mwaka wa 2019.
Ilipofika siku ya pili, uchovu ulikuwa umeanza kuingia huku Hilda akihangaika kusimama wima na kupika.
Kemem, ambaye alimtazama Hilda katika msururu huo wa mapishi kwa umakini namna alivyo jinyoosha kiuno na miguu yake kwa maumivu, alikuwa tayari kumfikia kumpa usaidizikwa dharura, alisema kuna hofu kwamba angeweza kukata tamaa wakati wowote.
‘’ Tulikuwa na hofu kila usiku, siku zote nne, huo ulikuwa wakati wa wasiwasi zaidi. Kupitisha usiku hadi asubuhi,’’ Kemem alisema.
Aliendelea kusema, ‘’Tulikuwa na hofu kwani mgongo wake ulianza kuuma, na tulijua kwamba hatungeweza kufanya mengi kwani ukimpa dawa ya maumivu, ingempa usingizi na upishi huo ungekoma.''
'' Kulikuwa na wakati ambapo miguu yake ilitaka kushindwa kwa sababu alisimama kwa muda mrefu sana. Ilikuwa inatisha sana.’’ alisema Kemem.
Kemem alisema kuwa moyo aliokuwa nao wa ujasiri ulimwezesha kuendelea na ushindani huo.
‘’Tulikuwa tumefanyia kazi miguu yake, kwa hivyo ilikuwa na uwezo wa kuhimili changa moto yoyote.’’
Taasisi ya Guiness World Record ilitangaza rasmi kuwa Hilda Baci amejiunga na orodha maarufu ya raia wa kimataifa ambao wamefanya mambo ya ajabu mnamo Juni 14, 2023.
Hilda amemshangilia mpishi mwingine chipukizi katika jimbo la Ekiti, Nigeria, ambaye amesema atajaribu kuvunja rekodi ya Hilda ndani ya mwezi mmoja.
Kitabu cha kumbukumbu cha Guinness kinanukuu rekodi za ulimwengu wa wanadamu asili.
Kilichapishwa kwa mara ya kwanza 1955 na Guinness Brewery huko Ireland na tangu wakati huo kimekuwa moja ya vitabu vya marejeleo maarufu zaidi na kusomwa mara nyingi zaidi.
Watu binafsi au vikundi lazima wawasilishe uthibitisho kwa kitengo cha Rekodi za Dunia cha Guinness na kupitia mchakato wa uthibitishaji ili kuhitimu kuorodheshwa kwa rekodi ya dunia.
‘’Ninajivunia sana Hilda, na ninahisi kupewa heshima kuu kwa kunihusisha sehemu ya safari hii,’’ mkufunzi wa mazoezi ya viungo Kemem alisema.