Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ameipongeza timu ya raga ya nchi hiyo, Springboks kwa ushindi wao wa Kombe la Dunia la Rugby 2023 dhidi ya New Zealand ambao unaifanya Afrika Kusini kuwa nchi ya kwanza kutwaa ubingwa huu mara nne.
"Kuimarika Pamoja ni imani ambayo ilikuja kuwa hai kwa wafuasi wa Springbok kote nchini na bara letu, na ulimwengu," Ramaphosa alisema katika taarifa baada ya mechi ambayo aliitazama kwenye Uwanja wa Stade de France mjini Paris.
"Usiku wa leo, Siya Kolisi na mabingwa wa Kombe la Dunia 2023 wametuzawadia mafanikio ya ajabu, ya kutia moyo na ambayo yanainua mioyo yetu na kuinua Bendera yetu juu zaidi," Rais Ramaphosa aliongeza.
Kocha wa Afrika Kusini Jacques Nienaber pia alielezea timu yake iliyoshinda Kombe la Dunia kama "mashujaa" na akasema uzoefu wao ulithibitisha tofauti katika ushindi wa 12-11 katika fainali Jumamosi dhidi ya New Zealand na kuhifadhi taji.
Nguvu ya kikosi
Afrika Kusini, timu ya kwanza kushinda Kombe la Dunia mara nne, iliwashinda wachezaji 14 wa kikosi cha ALL Blacks cha New Zealand katika pambano kali lililotoa cheche kwa mkwaruzano wa pembe za mafahali.
"Nadhani jambo kuu lilikuwa uimara wa kikosi," kocha huyo alisema.
"Wana uzoefu, wamewahi kucheza fainali ya Kombe la Dunia hapo awali, baadhi yao walikuwa wakicheza Kombe la Dunia la tatu. Kwa hivyo nadhani uzoefu ndio umefanikisha, ni kundi la watu wa ajabu, mashujaa wote.''
"Tumetoka mbali sana na wachezaji hawa, tumepanga kwa hili tangu 2018," aliongeza Nienaber, ambaye anaondoka kuchukua ajira mpya nchini Ireland baada ya mashindano nchini Ufaransa.
Ulikuwa ushindi wa tofauti ndogo zaidi dhidi ya wapinzani wao wa jadi ambao walipigana licha ya kupoteza.
"All Blacks walituhangaisha sana, inaonyesha tu ni timu gani, walipigana, walituweka chini ya shinikizo kubwa," alisema nahodha wa Springbok Siya Kolisi. "Sifa kwa kikosi changu kwa pambano, ninashukuru tu." aliongezea.