Mwezi

Na Dayo Yussuf

Kila mwezi wa 9 wa Kalenda ya Kiislamu, Ramadhani inarudi mzunguko mwingine. Mwezi wa mfungo unaozingatiwa na Waislamu zaidi ya bilioni 2 na nusu duniani kote.

Huu ni wakati ambao Waislamu wanajizuia kula na kunywa kuanzia alfajiri hadi jioni, huku wakimshukuru Mwenyezi Mungu kwa sala na kuzidisha ibada.

Na muda umewadia tena. Gumzo duniani kote ni kuhusu kuanza kwa mwezi wa mfungo na ibada.

Ramadhani ni nini?

Kwa mujibu wa Kitabu kitakatifu cha Waislamu, Quran, hii ni aina ya ibada iliyowekwa kwa wote kama ilivyokuwa kwa vizazi vilivyotangulia.

‘’Enyi mlioamini, Mmefaradhishiwa Saumu kama walivyokuwa wale kabla yenu ili mpate (kuwa) wema.” Inasema Aya ya Sura ya Ng’ombe ndani ya Quran. (Baqarah: 183)

Kwa mujibu wa wanazuoni wa Kiislamu, kufunga katika mwezi wa Ramadhani ni lazima lakini ni kwa manufaa ya mtu binafsi.

‘’Kwa Waislamu huu ni mwezi wa kuomba msamaha kwa Mungu kwa mapungufu yao.

Lakini pia wanatumia fursa hii kuweka mambo sawa na familia zao na marafiki na jamii nzima,’’ anasema Sheikh Shaaban Ismail, mwalimu wa dini ya Kiislamu jijini Nairobi. ‘’Waislamu wote walio katika umri wa balehe na kuendelea wanatakiwa kufunga isipokuwa wachache,’’ Sheikh Shaaban anaiambia TRT Afrika.

Nguzo za Uislamu

Swaumu ya Ramadhani imeorodheshwa kuwa moja ya nguzo tano zinazomkamilisha Muislamu.

Na nguzo hizo ni: ‘Shahada,’ tamko la kwamba hapana Mola anayepaswa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, na kwamba Muhammad ni mjumbe wake.

Ya pili ni sala tano kwa siku. Ya tatu ni Saumu ya mwezi wa Ramadhani, kisha Kutoa Zaka au sadaka na ya mwisho ni kwenda Makka kuhiji kwa wenye uwezo.

Kufunga katika mwezi huu wa Ramadhani ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Waislamu wote lazima waifuate. Wazazi huwafundisha watoto wao kuanzia umri mdogo ikiwezekana miaka saba au nane.

Vyakula vya kukaanga na vyakula vya mafuta mengi kama chips, sambusa, biriyani, pilau na kadhalika vinafaa kuepukwa kwa sababu vina calories nyingi na virutubisho vichache hivyo kusababisha mlo uwe usio na uwiano./Picha: Getty

‘’Baadhi ya wale ambao wamesamehewa mfungo ni wale wazee sana na watu wenye maradhi yasiyotibika. Badala yake wanapaswa kulisha maskini mlo wa kila siku katika mwezi huo,’’ Sheikh Shaaban anasema.

‘’Lakini ukipata maradhi ya muda, au ukiwa safarini, au wanawake wajawazito, au wanaonyonyesha na pia wale walio katika kipindi chao cha hedhi, wamesamehewa ingawa watalazimika kulipa kwa kufunga siku zote walizokosa,’’ anaongeza Sheikh Shaaban.

Faida kwa Waislamu na wasiokuwa Waislamu

Saumu ya Ramadhani sio tu kuacha kula na kunywa, pia unapaswa kujiepusha na matamanio ya kibinafsi na starehe, vitu kama kucheza muziki na kucheza densi, vitu ambavyo vinatazamiwa kuwa upotezaji wa wakati au usio na faida. Pia mfungaji ajiepushe na tendo la ndoa kwa muda wote alio funga mpaka atakapomalziza saumu yake jioni.

Lakini jinsi Waislamu wanavyoutarajia mwezi huu, ni dhahiri, kwa miaka mingi Wasio Waislamu wametambua umuhimu wake na wengine pia hutegea kwa hamu kubwa kufika kwake.

‘’Waislamu wakati wote wanatarajiwa kujiepusha na shughuli yoyote inayochukuliwa kuwa ni dhambi au isiyofaa. Lakini katika mwezi huu, wao huzidisha amali zao zote nzuri na huepuka starehe zozote ambazo wanaweza kufikiria vinginevyo. Hili nalo limethibitika kuleta amani na ustawi zaidi kwa jamii,’’ snasema Sheikh Shaaban.

Lakini pia ni pale watu wanapohitaji kuzidisha imani zao kwa kuabudu zaidi, kuonesha hisani na ukarimu wa hali ya juu na ndio maana utaona watu wengi wakiwaalika ndugu, jamaa na marafiki zao kufuturu pamoja nao kwa chakula kiitwacho 'iftari'.

Na kwa hakika watu wengi wanajua mlo huu kwa kawaida ni wa kipekee, ukiwa na mchanganyiko wa vyakula vitamu wakati mwingine huonekana ndani ya Ramadhan.

Waislamu na wasio Waislamu, ukipata mwaliko wa kula iftari na marafiki zako, ukubali mwaliko huo kwa tabasamu kwani ni baraka kwako na kwao pia.

Kutoka TRT Afrika, Tunakutakia Saum Makbul.

TRT Afrika