Mwezi Mtukufu wa Ramadhan umeanza wiki hii huku mamilioni ya Waislamu duniani kote wakikabiliana na mfumuko wa bei.
Utafiti uliofanywa na Statista kuhusu mwezi wa Ramadhan kwa mwaka 2021, unaonesha kuwa asilimia 35 ya watu waliohojiwa kutoka Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini waliweka wazi mabadiliko katika utaratibu wao wa kila siku, hasa wakati wa kufunga, kutokana na kuongezeka kwa bei ya bidhaa muhimu za chakula.
Kwa upande wake, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linakadiria kuwa watu milioni 349 katika nchi 79 walikuwa na ukosefu mkubwa wa chakula mwaka 2022 na zaidi ya milioni 140 walihitaji msaada, na idadi hiyo haitarajiwi kubadilika hivi karibuni.
Waislamu wengi Afrika wako tayari kufunga na wanafanya hivyo kama kutekeleza amri ya Mungu bila kujali changamoto zinazokuja na mwezi huo.
Hali ya Uchumi
“Hali ya kiuchumi imekuwa mbaya kutokana na ongezeko kubwa la bei hasa wakati huu wa mfungo,” amesema mkazi wa Dar es Salaam, Bi Shabani Asmani.
“Pilika pilika za biashara hupungua wakati wa mwezi wa Ramadhan mpaka karibu na siku ya Eid, hali inapobadilika, kwa mfano nauza jogoo wa Tabora kwa 40000 (dola 16) wakati wa sikukuu ila siku za kawaida nauza 25000 (dola 9),” Ali Maliza anasema.
Mabadiliko ya mlo
Baadhi ya familia zimelazimika kupunguza milo yao na huduma nyengine kutokana na ongezeko la bei wakati wa mwezi wa Ramadhan.
“Baada ya daku yenyewe hatuli, ukienda kufuturu ndio imepita mpaka kesho kutokana na hali ngumu ya uchumi,” Salum Said, anaielezea TRT Afrika.
Mfaume Omari, ambae ni dereva wa bodaboda kutoka Sinza, jijini Dar es Salaam, Tanzania, nae anasema yeye hushindia magimbi na tambi kwa wiki nzima ili kukwepa maumivu wa ugumu wa maisha katika kipindi cha mfungo.
“Kila sehemu tunayokimbilia kipindi hiki ni shida, sio kwenye vyakula wala mafuta, kama kilo ya nyama kwa sasa ni shilingi 8000 (dola 3), wakati wa Eid itakuaje,” anahoji Omari.
Wengi wanaamini kwamba kadri sikukuu ya Eid itavyokaribia, ndivyo bei zitakavyozidi kupanda kwani wafanyabiashara hukiona ni kipindi kizuri kuvuna zaidi kutoka kwa wateja na kutumia fursa ya siku hizo maalumu.
“Pamoja na changamoto zote hizi, lazima funga iendelee. Ni dhahiri kwamba bei za bidhaa zimepanda, kikubwa ni kujiandaa tu,” anaeleza Suleiman Omari, mkazi mwengine wa Dar es Salaam.
Hata hivyo, kuna matumaini kutoka kwa baadhi kwamba kuelekea mwisho wa mwezi mtukufu kutakuwa na unafuu kidogo.
“Si unaona mara nyingi vitu vinapanda bei siku za mwanzoni, lakini hali hubadilika kutokana na mshikamano wetu wa kidini,” anasisitiza Salum.