Vita nchini Sudan tangu Aprili 2023 vimelazimisha wengi kuhama makazi yao na hata walio nyumbani hawawezi kupata huduma inayohitajika kwa Ramadhan / Photo: AFP

Coletta Wanjohi

Instabul, Turkiye

Waumini wa dini ya kiislamu wanaanza kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhan, ambao ni mwezi unaonasibishwa na kufunga lakini vile vile kuwekeza muda mwingi katika kufanya ibada mbalimbali, ikiwemo kuswali na kusoma kitabu kitukufu cha Qur’an.

Hata hivyo, kutokana na vita vinavyoendelea nchini Sudan, mamilioni ya raia wa nchi hiyo, wanahofiwa kukosa fursa ya kufanya ibada ipasavyo.

Sudan ni nchi ambayo, zaidi ya asilimia 90 ya raia wake ni Waislamu. Lakini kutokana na hali tete inayoendelea nchini humo, wengi watakosa utulivu wa kushiriki kikamilifu katika ibada ya swaum.

Wengi wanawaza usalama wao.

Vita vinavyoendelea ni kati ya Jeshi la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na kikundi cha Rapid Support Forces RSF kinachoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo vimenoga tangu Aprili 2023.

Jeshi la Sudan linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan ( kushoto) limekataa wito wa kusimamishwa kwa vita wakati wa Ramadhan huku kikundi cha RSF kinachoongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo kilikuwa kimekubali wito huo. / Picha: Wengine.  

Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zimetoa wito kwa pande zinazopigana nchini humo kusitisha vita katika mwezi wa Ramadhan.

Kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) kilisema kinakaribisha wito wa kusitisha mapigano lakini upande wa jeshi la Sudan umekataa.

Yasser al-Atta, naibu kamanda wa jeshi la Sudan amefutilia mbali mapatano ya mwezi mtukufu wa Kiislamu wa Ramadhan akisema kuwa haitawezekana hadi kundi la wanamgambo wa RSF liondoke katika maeneo ya raia na umma.

Uongozi wa jeshi pia umesema lazima kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana kama Hemedti, aondolewe bila kupewa jukumu lolote yeye au familia yake, katika siasa za baadaye za Sudan au kijeshi.

Vita kati ya jeshi la Sudan na RSF ni mvutano kuhusu mpango wa mpito kwa utawala wa kiraia.

Pande hizo mbili zilifanya mapinduzi mwaka wa 2021 ambayo yalizuia mabadiliko ya awali kufuatia kupinduliwa kwa kiongozi wa zamani wa kiimla Omar al-Bashir mwaka wa 2019.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 14,000 tayari wamepoteza maisha kutokana na vita hivyo vinavyoendelea.

Huku zaidi ya watu milioni 8 wamelazimika kuhama makazi yao, kati yao takriban milioni mbili wamekimbilia nchi jirani za Chad, Sudan Kusini, Ethiopia na Uganda. Wengi wao, watashindwa kufunga kutokana na ugumu wa maisha ikiwemo ukosefu wa lishe.

Hata kwa wale zaidi ya milioni 6 walio bado nchini hawana uwezo wa kupata mahitaji muhimu ikiwemo sehemu za kufanya ibada na chakula cha kuwakidhi. Umoja wa Mataifa tayari umetahadharisha kwamba, misaada ya kibinadamu haiwezi kufika katika maeneo ya vita.

Kadri siku zinavyokwenda, ndivyo jitihada za kuleta suluhu zinavyozidi kugonga mwamba tangu Mei 2023.

TRT Afrika