Rais anayemaliza muda wake Julius Maada Bio amechaguliwa tena kwa muhula wa pili / Picha ya AFP

Rais wa Sierra Leone Maada Bio ameapishwa kwa muhula wake wa pili saa chache baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza kuwa mshindi.

Kulingana na katiba ya Sierra Leone, mshindi wa uchaguzi wa urais lazima aapishwe siku hiyo hiyo wanapotangazwa kuwa washindi.

Sherehe ya kuapishwa kwa Rais Bio ilifanyika katika Ikulu mara tu baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza kuwa mshindi katika tangazo lililotolewa Jumanne.

"Kwa mamlaka niliyopewa... hapa ninatangaza kuwa Bio Julius Maada... [ame]chaguliwa rasmi kuwa rais," alitangaza Kamishna Mkuu wa Uchaguzi Mohamed Konneh, licha ya pingamizi kutoka upinzani.

Rais kisha alitoa hotuba akishukuru wananchi kwa "imani na ujitoaji wao," akiongeza kuwa "ushindi huu ni wa kila Msierra Leone." Chama cha Rais Bio, Sierra Leone People's Party (SLPP), kilishinda karibu kura milioni 1.6 - sawa na 56.1% ya kura zote.

Matokeo Yaliyopingwa

Ushindi wake hata hivyo umepingwa na mpinzani wake Samura Kamara ambaye alipata asilimia 41 ya kura kupitia Chama cha All People's Congress (APC).

APC ilikataa matokeo ya muda yaliyoonyesha uongozi wa awali kwa Bio siku ya Jumatatu, ikielezea matokeo hayo kuwa "takwimu zilizopikwa."

APC ilidai kukosekana kwa uwazi na uwajibikaji kutoka kwa tume ya uchaguzi katika kuhesabu kura, na kuongeza kuwa mawakala wake "hawakuruhusiwa kushiriki (katika vituo vya kuhesabu) wala hawakuruhusiwa kuthibitisha matokeo kabla ya tangazo."

Hesabu ya kura ilikuwa na mvutano na utata huku baadhi ya waangalizi wa kimataifa wakiwasilisha wasiwasi kuhusu uadilifu wa mchakato huo.

"Waangalizi wa Kituo cha Carter waliripoti kuwa mchakato wa kuhesabu ulikosa kiwango cha kutosha cha uwazi," kundi la waangalizi lilisema katika taarifa kabla ya tume ya uchaguzi kutangaza matokeo ya mwisho.

TRT Afrika