Rais wa Nigeria Bola Tinubu alitia saini mswada wa kima cha chini cha mshahara kuwa sheria katika jumba la kifahari la rais katika mji mkuu Abuja mnamo Julai 29, 2024. / Picha: TRT Afrika

Rais wa Nigeria Bola Tinubu ametia saini mswada wa kima cha chini cha mshahara kuwa sheria.

Sheria mpya inaweka kima cha chini cha mshahara wa kitaifa kuwa naira 70,000 ($45), kutoka naira 30,000 ($20) hapo awali.

Mnamo Julai 18, serikali na mwavuli wa vyama vya wafanyikazi nchini Nigeria walikubaliana juu ya kima cha chini cha mshahara baada ya vikundi vya kushawishi kuapa kuandamana ikiwa serikali itakataa kuongeza malipo ya kima cha chini.

Vyama vya wafanyakazi vilikuwa vimeshinikiza kuboreshwa kwa kima cha chini cha mshahara, vikitaja gharama kubwa ya maisha inayotokana na mfumuko wa bei na bei ya juu ya mafuta.

Maandamano

Rais Tinubu alitia saini mswada wa kima cha chini cha mshahara kuwa sheria katika jumba la kifahari la rais katika mji mkuu Abuja siku ya Jumatatu.

Kiwango kipya cha chini cha mshahara, kilichotiwa saini wakati wa uhamasishaji wa maandamano unaendelea, kinatumika kwa majimbo yote 36 ya Nigeria.

Raia wa Nigeria waliohuzunishwa wanapanga kuandamana kuanzia Agosti 1 kuhusu kile wanachoita "utawala mbovu."

TRT Afrika