Rais wa Namibia, Hage Geingob, amewashukuru wananchi wa Namibia na watu wema baada ya kufanyiwa matibabu ya moyo katika nchi jirani ya Afrika Kusini.
Alifanyiwa kile ambacho ofisi ya rais wa Namibia ilieleza kama upasuaji ''mdogo'' baada ya kugundulika kuwa ana dalili za awali za ugonjwa wa stenosis kwenye mishipa ya moyo ambayo huzuia mtiririko wa damu, ofisi ya raisi ilisema.
Rais huyo, 81, alitibiwa nchini Afrika Kusini kwa sababu huduma hiyo haikupatikana nchini humo na anatarajiwa kurejea kazini siku ya Jumanne, iliongeza.
Geingob alitweet Jumapili kuhusu "shukrani zake za dhati kwa jumbe za kutia moyo" alizopokea katika kipindi hicho.
"Ninawashukuru Wanamibia, viongozi wa kisiasa, ndugu na marafiki kutoka duniani kote kwa salamu za heri baada ya upasuaji wangu tarehe 10 Juni 2023. Siwezi kujibu kila ujumbe. Muwe na uhakika wa shukrani zangu za dhati kwa jumbe zote za kutia moyo katika kipindi hiki chote.
Geingob anahudumu muhula wake wa pili baada ya kuingia madarakani katika uchaguzi wa urais wa Novemba 2014.
Hastahiki kugombea katika uchaguzi ujao wa urais unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao.