Rais wa Malawi Lazarus Chakwera, siku ya Alhamisi amemteua Michael Bizwick Usi kama makamu wake, akichukua nafasi ya Saulos Chilima, aliyefariki dunia kwa ajali ya ndege hivi karibuni.
Akiwa ni mtunzi wa vitabu vya tamthiliya, muigizaji na mwanaharakati wa haki za kiraia, Usi amehudumu kama Makamu wa Rais wa chama cha Chilima cha United Transformation Movement (UTM), toka kuanzishwa kwake 2018.
Alichaguliwa kwenye baraza la mawaziri la Chakwera mwaka 2020 wakati UTM ilipoamua kushirikiana na chama cha Chakwera cha Malawi Congress Party (MCPP) kwenye uchaguzi wa mwaka 2020.
Kielimu, mwanasiasa huyo mwenye miaka 56, ana shahada mbili za Uzamili katika usimamizi wa kimkakati na maendeleo ya kimataifa. Pia, ana shahada ya uzamivu kwenye maendeleo ya vijana.
Kuapishwa
Kabla ya kujishughulisha na siasa, Usi alifanya kazi za maendeleo katika vyama visivyo vya kiserakali.
Anatarajiwa kuapishwa siku ya Ijumaa katika mji mkuu wa Malawi, Lilongwe.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamepongeza hatua hiyo katika "mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo."
'Ishara ya ukomavu'
George Phiri aliiambia Anadolu kuwa uteuzi wa Usi ni "ishara dhahiri" kuwa Rais Chakwera amethamini kazi ya Chilima.
"Uteuzi huu, bila shaka yoyote unaonesha namna gani Rais Chakwera ameguswa na kifo cha Chilima. Hii itaimarisha umoja wa kisiasa ulioanza kuyumba. Nampongeza sana Rais kwa ishara hiyo ya ukomavu," Phiri amesema.
Malawi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwezi Septemba mwakani, huku hali ya joto la kisiasa ikizidi kupanda.