Rais wa Kenya William Ruto, amesema kuwa njia zote zinazohitajika, zitumike ili kuhakikisha kuwa michakato ya kidemokrasia inadumishwa barani Afrika huku akiunga mkono juhudi za muungano wa ECOWAS na afua wanazoweka ili kutatua hali ya Niger.
Kwenye kikao na waandishi wa habari huku akiendelea na ziara yake nchini Msumbiji, Ruto amekaribisha juhudi za ECOWAS kuhusiana na Niger huku akisema kuwa Afrika, inahitaji kulindwa kutoka kwa wale aliowataja kuwa 'kutumia pipa la bunduki kuendesha mambo ya nchi na kusimamia masuala ya bara letu na kupinga mteremko wa udikteta wa kijeshi na kuondolewa kwa serikali za kiraia kinyume na katiba.
"Afrika ni bara la kidemokrasia na lina sifa za kutosha za kidemokrasia kuweza kusimamia mambo ya nchi zetu kwa uhalali unaotokana na uamuzi wa wananchi katika chaguzi za kidemokrasia." Alisema.
Juhudi za kuleta amani Sudan
Wakati huo huo, Ruto amezungumzia juhudi zinazoendelea kusuluhisha mzozo wa Sudan na kusema kuwa kama kanda ya Afrika Mashariki, wanafanya kazi kwa pamoja chini ya mipango mbalimbali kama vile mpango wa Jeddah, mfumo wa IGAD-AU na pia kupitia mfumo wa majirani chini ya uenyekiti wa Misri, ili kurejesha utulivu nchini humo.
"Hii leo nilizungumza na aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani wa Sudan, Hamdok, ambaye ni miongoni mwa watu wanaoongoza vikundi vya kiraia vinavyoshirikisha pamoja vyama vya kisiasa, mashirika ya kiraia, vikundi vya wanawake, na vijana ili kufanikisha mfumo wa jinsi ya kutatua masuala ya Sudan na kuipeleka nchi mikononi mwa utawala wa kiraia na wa kidemokrasia." Aliongeza
Rais huyo wa Kenya ameongeza kuwa amezungumza na Marais wa Ethiopia, Misri na Chad chini ya ushirikiano wa AU-IGAD ili kutatua mgogoro unaoendelea Sudan huku akitaja kuwa mzozo unaoshuhudiwa Sudan unastahili kusuluhishwa haraka iwezekanavyo kwani maafa na uharibifu wa mali na miundombinu inayoendelea, haikubaliki kwa njia yoyote ile.
Tusiruhusu mbadiliko ya kitawala usio halali
Rais huyo wa tano wa Kenya ametoa wito kwa Afrika kuunga mkono chaguzi za kidemokrasia kwani ndio mabadiliko pekee ya kiserikali yatakayofanikisha matarajio ya nchi na watu wa bara la Afrika.