Rais wa Nigeria Bola Tinubu amechaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS.
Tinubu, 72, alichaguliwa tena wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi wa ECOWAS katika mji mkuu wa Nigeria Abuja siku ya Jumapili.
Kiongozi huyo wa Nigeria anaendelea kushikilia kiti hicho licha ya baadhi ya nchi wanachama wanaozungumza Kifaransa kuripotiwa kupinga kuchaguliwa kwake tena.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) inakabiliwa na changamoto kubwa, ikiwa ni pamoja na kuondoka kwa nchi tatu wanachama - Burkina Faso, Mali na Niger - pamoja na tatizo la kifedha.
Ukosefu wa usalama
Ukosefu wa usalama katika baadhi ya mataifa wanachama umeifanya ECOWAS kufikiria kuanzisha kikosi cha kikanda ambacho kitajitolea kukabiliana na tatizo la kudumu la uasi, ambalo limegharimu maisha ya maelfu ya watu.
Jumuiya hiyo ina jumla ya watu milioni 425, lakini kwa kuondoka kwa nchi tatu zilizojitenga, shirika la kikanda litapoteza kundi la watu wapatao milioni 72.
Mwenyekiti wa ECOWAS anateuliwa na wakuu wengine wa nchi na serikali kusimamia masuala ya jumuiya hiyo kwa muda wa mwaka mmoja.