Rais wa Kenya WIlliam Ruto na mwenzake wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wamethibitisahwa kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa Paul Kagame kama Rais wa Rwanda kwa uhula wake wa nne.
Takriban wakuu 23 wa nchi na serikali wanatarajiwa kuhudhuria kuapishwa kwake baada ya kutwaa ushindi wa 99% katika uchaguzi uliofanyika Julai 15.
Kagame, 66, ambaye aligombea chini ya tikiti ya chama tawala cha Rwandan Patriotic Front (RPF), aliwashinda kwa kishindo wapinzani wake wawili - Frank Habineza wa Democratic Green Party of Rwanda na mgombea binafsi Philippe Mpayimana.
Hata hivyo ofisi ya kurugenzi ya mawasiliano ya Rais Kagame imesema kuwa Rais Museveni atawakilishwa na mwanaye ambaye ndiye pia mkuu wa jeshi Jenerali Muhoozi Kainerugaba.
Sherehe ya uzinduzi, inayotarajiwa kufanyika katika Uwanja wa kisasa wa Amahoro katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali, itakaribisha takriban watu 40,000.
Mbwembwe zitaambatana na densi za kitamaduni, gweride la kijeshi na mambo muhimu mengine ya kitamaduni.