Rais Paul Kagame wa Rwanda amesisitiza haja ya kuwekeza kwa vijana walioko kwenye nchini za Umoja wa Jumuiya za Madola.
Hatua hiyo inalenga kutatua changamoto mbalimbali ulimwenguni, kulingana na Rais Kagame.
Rais Kagame ametoa kauli hiyo siku ya Oktoba 25, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 27 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) unaofanyika jijini Apia, nchini Samoa.
“Utengenezwaji wa ajira za kidijiti kwa wanawake na vijana iwe ni kipaumbele kwa mwaka huu,” alisema Kagame, akisisitizia umuhimu wa kuwezesha vikundi hivyo.
Kulingana na Kagame, faida za nchi za Jumuiya ya Madola zinapatikana kwa idadi ya vijana.
“Faida za nchi za Jumuiya ya Madola zipo kwa vijana hawa wenye nguvu na ari.”
Kiongozi huyo pia aligusia changamoto mbalimbali kama ongezeko la ukosefu wa ajira na uhamaji usio wa kawaida, akionya kuwa mambo hayo yanatishia hali ya utulivu kati ya mataifa.
Pia, aliwataka viongozi kuendelea kutegemea ubunifu na teknolojia kutatua changamoto ya ongezeko la ukosefu wa ajira.
Kwa namna ya pekee, Rais Kagame aligusia matumizi sahihi ya Akili Mnemba, akitoa wito wa uwepo wa sera madhubuti za kudhibiti eneo hilo.