Rais Paul Kagame ambaye pia ni mgombea wa chama cha Rwanda Patriotic Front (RPF) kwenye uchaguzi ujao wa urais amewasilisha nyaraka zake kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Hatua hiyo inakuja wakati NEC imeanza rasmi kupokea taarifa za wagombea kutoka kwa watu wanaotaka kugombea uongozi wa juu wa nchi hiyo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Julai 15, 2024.
Kulingana na tume hiyo, wagombea 8 wameonesha nia ya kuwania kiti cha Urais kama wagombea binafsi.
"Jalada lake limekamilika," mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa nchi hiyo, Oda Gasinzigwa alisema baada ya kupokea nyaraka za Rais Kagame.
Kagame alichaguliwa na RPF kuwakilisha chama hicho katika uchaguzi wa Machi 9, 2024 baada ya kumshinda Sheikh Abdul Karim Harerimana kwa asilimia 99.1.
Kagame ni rais wa awamu ya nne wa nchi akiwa ameiongoza Rwanda toka mwaka 2000.
Sifa za wagombea
Kulingana na NEC, ili ugombee Urais wa nchi hiyo, ni lazima uwe Mnyarwanda na uwe na mzazi angalau mmoja aliyezaliwa nchi hiyo.
Sharti lingine ni kuwa lazima uwe umetimiza walau miaka 35, na kuonesha uadilifu wa hali ya juu katika jamii zao.
Wanapaswa kuonesha ushahidi wa kutokuwa na historia yoyote ya kuhukumiwa kwa makosa ya jinai yenye kupelekea vifungo vinavyozidi miezi sita.
Tume hiyo imesisitiza kuwa ni lazima kwa watia nia hao kuwasilisha nyaraka zao kama maombi ikiwa ni pamoja na barua iliyotumwa kwa rais wa tume ya uchaguzi, kueleza nia ya mtu binafsi kugombea nafasi ya urais, cheti cha kuzaliwa cha mgombea na uthibitisho wa uraia wa Rwanda, kutoka Idara ya Uhamiaji ya nchi hiyo.
Kulingana na tume hiyo, watia nia ambao awali walikuwa watumishi wa umma na kuwahi kushika nyadhifa nyingine serikalini, wanapaswa kutangaza mali zao na kwa NEC.
"Wagombea wanapaswa kuwasilisha hati zao zenye kuthibitisha kuwa wao ni raia wa Rwanda," ilisema NEC.
Iwapo hapo awali walikuwa na uraia wa nchi nyingine, wanapaswa kuwasilisha hati zinazoonyesha kuwa wamezikana.
Kwa wagombea wanaowakilisha vyama vya siasa, wanapaswa kutoa hati za uidhinishaji kutoka kwa chama chao cha kisiasa, kuthibitisha kwamba walikuwa mbele ya wagombea hao.
Kwa wagombea binafsi, NEC inawataka kuwasilisha angalau saini 600 kutoka kwa wananchi kote nchini, kuidhinisha ugombea wao.