Mahakama ya Paris Jumatano ilimpata na hatia Philippe Hategekimana, polisi wa zamani wa kijeshi wa Rwanda, kwa mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinadamu wakati wa mauaji ya mwaka 1994 nchini Rwanda na kumhukumu kifungo cha maisha gerezani.
Mahakama ilisema imempata Hatagekimana, 66, na hatia katika karibu na mashitaka yote dhidi yake.
Aliikimbia Rwanda baada ya mauaji ya kimbari, akapata hadhi ya mkimbizi na kisha uraia wa Ufaransa chini ya jina la Philippe Manier.
Kesi ya Hategekimana, ambayo ilianza mwezi uliopita, ilikuwa ni kesi ya tano kama hiyo nchini Ufaransa dhidi ya washukiwa wa mauaji hayo.
Zaidi ya watu 800,000 waliuawa kati ya Aprili na Julai 1994 kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, wengi wao wakiwa ni watu wa jamii ya Watutsi.
Washitaki walimtuhumu Hategekimana kwa "kutumia mamlaka na nguvu za kijeshi alizopewa kupitia cheo chake ili... kushiriki katika mauaji ya kimbari."
Hata hivyo, alikana mashtaka hayo.
Ufaransa, ambayo ni moja ya nchi zenye kuwavutia wahalifu wa mauaji hayo, imefanya kesi na kuhukumu aliyekuwa mkuu wa upelelezi, waliokuwa meya wawili, dereva wa zamani wa hoteli na afisa wa zamani wa ngazi ya juu katika kesi kama hizo tangu mwaka 2014.
Hata hivyo, mara nyingi imekataa ombi la kuwasafirisha washukiwa kwenda Rwanda, hali iliyosababisha Rais Paul Kagame wa Rwanda kuishutumu Paris kwa kukataa Rwanda kuwa na mamlaka ya kisheria.
Hategekimana alihamishwa kutoka Cameroon mpaka Ufaransa mwaka 2019, amekuwa kizuizini kwa muda tangu Februari 15, 2019.