Mkuu wa polisi wa Afrika Kusini ameomba msamaha hadharani kwa waathiriwa wanane wa ubakaji baada ya maelezo yao ya kibinafsi, ikiwa ni pamoja na majina, umri na anuani za makazi, kuishia kwenye mitandao ya kijamii.
Wanawake hao walibakwa mwaka jana walipokuwa wakipiga video ya muziki katika mgodi uliotelekezwa huko Krugersdorp, mji ulioko magharibi mwa Johannesburg.
Walivamiwa na genge la watu wenye silaha ambao pia waliwaibia wafanyakazi wa kutengeneza video. Uhalifu huo ulilaumiwa kwa wachimbaji haramu wa kigeni wanaochimba dhahabu katika migodi iliyofungwa, kulingana na ripoti za ndani.
Kamishna wa polisi Fannie Masemola alisema maelezo ya wahasiriwa hapo awali yalishirikiwa kwenye vikundi vya ndani vya WhatsApp ili kuwahamasisha maafisa kukamata lakini wakapata njia yao kwenye mitandao ya kijamii.
"SAPS inasikitika kufichuliwa kwa habari kama hizo za kibinafsi na inawaomba radhi waathiriwa wa uhalifu wa kutisha kwa uvunjaji wa habari na ugumu uliosababishwa na matokeo," alisema katika taarifa.
Uchunguzi wa ndani haukupata nia mbaya kwa upande wa maafisa.
"Hata hivyo hii bado haihalalishi ugawaji wa habari kama hizo," Bw Masemola aliongeza.
Zaidi ya washukiwa 80 walikamatwa kutokana na mashambulizi hayo lakini mashtaka yalitupiliwa mbali kwa kukosa ushahidi.
Ubakaji na wizi huo wa genge ulizua hasira ya umma nchini Afrika Kusini na waandamanaji walifanya maandamano nje ya mahakama ya Krugersdorp wakati washukiwa hao walipofikishwa mahakamani.