Coletta Wanjohi
Istanbul, Uturuki
Unapotembea nchini Afrika Kusini bila shaka utakutana na ndege aina ya Penguin.
Hawa ni ndege wa majini wasioweza kuruka.Kuna spishi moja ya ndege hawa inayoitwa penguin wa kiafrika, inayopatikana Afrika.
Hawa hupatikana tu kwenye pwani ya Kusini Magharibi mwa Afrika. Wapo pia Namibia, Gabon, Msumbiji, Congo na Angola.
Penguin wa Kiafrika ni wadogo wakilinganishwa na spishi nyengine 17 za ndege hawa.
Wanaweza kutambuliwa kwa rangi yao ya pinki juu ya macho, ambayo hutumiwa kudhibiti joto la mwili.
Kadiri anavyopata joto, ndivyo damu inavyotiririka katika maeneo haya, ambapo hupozwa na hewa inayozunguka, na kumfanya kuhisi baridi.
Ndege hawa wanakuwa na mwenza mmoja tu katika maisha yao. Majike na madume hutoa sauti kama ya punda, kama njia ya mmoja kumvutia mwengine.
Jike hutaga mayai mawili, ambayo huwa tayari kutotolewa ndani ya siku 40.Baada ya hapo, jike na dume hupokezana majukumu ya kulea vifaranga. Majukumu hayo ni pamoja na kuwalisha na kuwalinda vifaranga mpaka watakapofika umri wa siku 30.
Kuanzia mwezi Mei hadi Agosti, ndio muda muafaka unaotumika na ndege hawa kuzaliana hasa kwenye ardhi yenye miamba yenye mimea midogo au pasipo na mimeo yoyote.
Penguin wana manyoya mazito yenye rangi nyeusi, nyeupe, na kijivu yasiyopitisha maji ambayo muda wote huwafanya wabaki na joto katika msimu wa maji baridi ya pwani ya Afrika.
Uhodari wao wa kuogelea, unawawezesha kukamata kwa urahisi aina mbalimbali ya mawindo kutoka baharini.
Wanaweza kushikilia pumzi zao kwa zaidi ya dakika 2 na kupiga mbizi zaidi ya futi 400 kwenda chini ya maji.
Penguin wa Kiafrika wanaweza kufikia urefu wa sentimita 60-68 na uzito wa kilo 3 hadi 4 huku madume wakiwa wakubwa kidogo kuliko majike.
Ndege hawa ni muhimu.
Mbali na kuwa kivutio cha utalii, wanasaidia katika ikolojia kama chanzo cha chakula cha papa huku nao wakiwinda samaki wadogo.
Hata hivyo, ndege hawa wapo hatarini. Wataalamu wanasema idadi yao inapungua kwa kasi kutokana na ushindani na uvuvi wa kibiashara na mabadiliko ya hali ya hewa.