Kwa wale ambao walikuwa nchini Kenya miaka ya tisini bila shaka wanamkumbuka Kamlesh Pattni, maarufu ‘Goldenberg scandal.’
Pattni wenye uraia pacha wa Kenya na Uingereza mwenye asili ya Asia, amejikuta kwenye sakata jengine ambapo serikali ya Uingereza na Marekani zimemuwekea vikwazo kwa madai ya kuhusika katika biashara haramu ya dhahabu na utakatishaji wa fedha.
Kufuatia vikwazo hivyo, mali ya Kamlesh Pattni na wengine wanne akiwemo mke wake na shemeji yake zitazuiliwa.
Jina la Kamlesh Pattni lilianza kupata umaarufu kimataifa kwa mara ya kwanza baada ya kashfa ya Goldenberg nchini Kenya katika miaka ya 1990, kashfa hiyo ilihusisha ulanguzi wa dhahabu iliyoibia Kenya yenye thamani ya dola milioni 600 katika kashfa ya Goldenberg.
Pattni alishtakiwa kwa ufisadi dhidi ya wanachama wengi wa serikali ya Rais wa wakati huo Daniel Arap Moi.
Baada ya miaka mingi ya kushtakiwa, Pattni aliachiliwa baada ya kukana makosa yote. Kuanzia mwaka 2002, Pattni alifunguliwa mashtaka na kufikishwa mahakamani, lakini kesi zilisambaratika.
Baadaye Pattni alijipachika wadhifa wa mchungaji wa kidini. Patnni alitoroka na kuelekeza makazi yake nchini Zimbabwe. Nchini Zimbabwe, Pattni alifanya urafiki na Rais wa wakati huo Robert Mugabe na kuanzisha tena mpango unaofanana na ule aliokuwa nao Kenya.
Pattni, kama inavyoonyeshwa katika ripoti za umma na kwengineko, alifanya shughuli zake kwa kushirikiana na watu mbalimbali katika kufanikisha biashara zake zinazodaiwa kuwa ni za haramu kutoka Zimbabwe.
Baada ya kuuza maliasili za Zimbabwe katika nchi za kigeni, alidaiwa kushirikiana na wenzake katika kuiibia serikali kwa kuleta mapato chini ya kiwango.
Pattni anashtakiwa kuficha faida kupitia mtandao wa kimataifa ya makampuni yalioonekana kuwa halali.