Papa Francis amemfukuza kazi kasisi wa Rwanda anayetuhumiwa kupanga mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi katika taifa hilo la Afrika mashariki.
Askofu Christian Nourrichard alisema uamuzi wa kumwondoa Munyeshyaka haukupaswa kukata rufaa.
Gazeti la The New Times la Rwanda linaripoti kwamba Munyeshyaka anashukiwa kuongoza mauaji ya kimbari katika maeneo tofauti ya Kigali, hasa katika Kanisa Katoliki la Saint Famille, ambako alikuwa kasisi mwaka 1994.
"Kwa amri ya Machi 23, 2023, iliyopokelewa wiki iliyopita, Baba Mtakatifu Francisko, kwa uamuzi wake mkuu na wa mwisho, ambao hauhusiani na rufaa yoyote, amefutilia mbali pœnam ya ukasisi kwa Padre Wenceslas Munyeshyaka, wa Jimbo kuu la wa Kigali (Rwanda) na kwa sasa anaishi Dayosisi ya Evreux,” Askofu Nourrichard alisema katika notisi hiyo ya Mei 2.
"Padre Wenceslas Munyeshyaka ameondolewa katika majukumu yote yanayotokana na kuwekwa wakfu, moja kwa moja anapoteza haki zote maalum kwa taasisi ya ukasisi, ametengwa na huduma takatifu na hawezi kufanya kazi kama mhadhiri au msaidizi, wala kufanya ushirika popote. Anapaswa kuepuka maeneo ambayo hadhi yake ya awali inajulikana."
Mnamo Desemba 2021, askofu wa Evreux alimsimamisha kazi Munyeshyaka ya majukumu ya ukasisi baada ya kudaiwa kuwa alipata mtoto nje ya ndoa kinyume na desturi za kanisa.
Mwaka 2006, alipatikana na hatia ya uhalifu wa mauaji ya kimbari bila kuwepo mahakamani na mahakama za Gacaca nchini Rwanda.
Alikabiliwa na mashtaka zaidi katika Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), lakini mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa baadaye ilipeleka kesi yake katika mahakama ya Ufaransa, ambayo iliitupilia mbali mwaka 2015.
Munyeshyaka alibaki nchini Ufaransa ambako aliendelea kuhudumu kama kasisi katika parokia tofauti, hadi aliposimamishwa kazi mwaka 2021 na Nourrichard.
Kasisi aliyeachishwa kazi bado hajatoa maoni yake kuhusu uamuzi wa Papa.