Mazungumzo hayo, ambayo yalisitishwa tangu Juni, yamepangwa kuanza kujadili makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano kote nchini humo, na kusaka njia za kuanza kwa mchakato wa kisiasa na ushiriki wa vikosi vya kisiasa na vya kiraia.
Jeshi la Sudan (SAF) ambalo liliondoka katika meza ya mazungumzo, limesema kuwa litaanza tena mazungumzo ya amani na vikosi vya kijeshi (RSF) Alhamisi wiki hii, huko mjini Jeddah, Saudi Arabia.
Naibu Kamanda wa jeshi la Sudan SAF, Shamseddine al-Kabashi, alitangaza kwamba jeshi lilialikwa Jeddah kuanza tena mazungumzo.
"Ujumbe wetu utaenda Jeddah na kuanza mazungumzo siku ya Alhamisi ijayo," aliwaambia maafisa wa jeshi katika kituo cha kijeshi cha Wadi Seidna, kule Omdurman.
"Mazungumzo yataanza kwa kuangazia masuala ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na utoaji wa msaada kwa maeneo ya vita. Awamu ya pili itahusisha majadiliano ya kusitisha mapigano, na hatua ya mwisho zitahusu njia ya kisiasa ya kujaribu kumaliza vita nchini, " alimaliza.
Maelfu ya watu wameuawa na mamia ya maelfu kujeruhiwa tangu vita hivyo vilipoanza nchini humo Aprili 15 mwaka huu kati ya SAF na RSF.
Upatanishi wa pande hizo unaoongozwa na Saudi Arabia na Marekani, ulisitishwa mapema mwezi juni baada ya vyama vya Sudan kushindwa kufuata makubaliano ya pili ya kusitisha mapigano na kuwezesha kuingia kwa misaada ya kibinadamu ili kuwafikia raia waliokwama katika maeneo ya mapigano huko Khartoum.