Pande zinazozozana nchini Sudan zimefikia makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku saba, Saudi Arabia na Marekani zilisema katika taarifa ya pamoja baada ya mazungumzo huko Jeddah.
Wawakilishi kutoka kwa mkuu wa majeshi Abdel Fattah al Burhan na naibu wake wa zamani aliyegeuka mpinzani Mohamed Hamdan Daglo waliapa kutotafuta manufaa yoyote ya kijeshi kabla ya kuanza kutekelezwa kwa mapatano saa 9:45 jioni saa za Khartoum [1945 GMT] mnamo Mei 22, taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema Jumapili.
Usitishaji mapigano "utaendelea kutekelezwa kwa siku saba na unaweza kuongezwa kwa makubaliano ya pande zote mbili," ilisema.
Usitishaji mapigano kama huo wa siku za nyuma haukuheshimiwa na pande zinazopigana.
Sudan imekumbwa na msukosuko tangu kuzuka kwa mzozo kati ya jeshi na Kikosi cha Msaada wa Haraka [RSF] katikati mwa Aprili.
Vifo vya watu wengi na wengine kupotezana
Siku ya Ijumaa, kiongozi wa kijeshi wa Sudan Burhan alimfukuza kazi Daglo, na kumpa cheo chake cha makamu wa rais wa Baraza Kuu tawala kwa kiongozi wa zamani wa waasi Malik Agar, na kuwateua washirika watatu kuchukua nafasi za juu katika jeshi.
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu hali ya kibinadamu inayozidi kuzorota kwa kasi katika nchi hiyo ya tatu kwa ukubwa barani Afrika, ambapo mtu mmoja kati ya watatu tayari alitegemea msaada kabla ya mzozo huo.
Makundi ya misaada yamesema hayawezi kutoa msaada wa kutosha mjini Khartoum, mji mkuu, kwa kukosekana kwa njia salama na dhamana ya usalama kwa wafanyakazi.
Mzozo huo ulioanza Aprili 15, umesababisha takriban watu milioni 1.1 kuyahama makazi yao ndani na katika nchi jirani.