Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina Riyad Al Maliki ameielezea mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa kuhusu "ukoloni na ubaguzi wa rangi" wanaopitia raia wa nchi hiyo chini ya utawala wa Israel, na kumuomba Jaji wa Mahakama hiyo kuamuru kuondolewa kwa umiliki wa wapalestina katika eneo hilo.
"Wameteseka vya kutosha na madhila ya ubaguzi wa rangi na ukoloni...kuna wanaoumizwa na maneno hayo mawili. Inabidi wachukizwe na yale tunayopitia," alisema Al Maliki siku ya Jumatatu.
Akizungumza mjini The Hague ilipo mahakama hiyo, waziri huyo aliiomba majaji wa taasisi hiyo ya haki kusitisha mara moja utawala wa kimabavu wa Israel ndani ya Palestina.
"Haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki iliyonyimwa na Palestina wamenyimwa haki hiyo kwa muda mrefu sana," amesema. "Ni wakati muafaka kuondoa utofauti huu uliowaweka watu wetu kifungoni kwa muda mrefu."
'Kutokujali na kutotenda'
Mnamo Desemba 2022, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliiomba ICJ "maoni ya ushauri" yasiyofungamana na "matokeo ya kisheria yanayotokana na sera na desturi za Israel katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki."
Maoni kutoka ICJ yanakuja nyuma ya shinikizo kubwa la kisheria kutoka jumuiya ya kimataifa kuhusu mashambulizi ya Israel dhidi ya eneo la Gaza.
Vikao hivyo ni tofauti na kesi ya hadhi ya juu iliyoletwa na Afrika Kusini inayodai kuwa Israel inafanya mauaji ya halaiki wakati wa uvamizi wa sasa wa Gaza
Hata hivyo, kulingana na Al Maliki, 'mauaji ya kimbari' yanayoendelea Gaza ni matokeo ya miongo mingi ya kutokujali wala kuchukua hatua.
"Suala la kumaliza ubabe wa Israel ni suala la kimaadili, kisiasa na ni lazima kisheria," alisema.
Mwezi Januari, Mahakama ya ICJ iliiamuru Israel kuzuia kuendelea kwa mauaji hayo na kuruhusu msaada wa kibinadamu kutolewa kwa waathirika.
Siku ya Ijumaa, ICJ ilikataa ombi la Afrika Kusini la kuweka hatua za ziada kwa Israel, lakini ikasisitiza haja ya kutekeleza uamuzi huo kikamilifu.
'Kukaliwa kwa muda mrefu'
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeitaka ICJ kuzingatia maswali mawili.
Kwanza, mahakama hiyo kupitia madhara ya kisheria wa kile kinachoitwa na Umoja wa Mataifa kama 'kuendelea kwa ukiukwaji wa haki za kibinadamu kwa watu wa Palestina".
Hii inahusiana na "ukaaji wa muda mrefu, makazi na kunyakua ardhi ya Palestina iliyokaliwa kwa mabavu tangu 1967" na "hatua zinazolenga kubadilisha muundo wa idadi ya watu, tabia na hadhi ya Mji Mtakatifu wa Jerusalem".
ICJ pia imetakiwa kuangalia matokeo ya kile ilichoeleza kama "kupitishwa kwa sheria na hatua za kibaguzi zinazohusiana na Israeli."
Mahakama itatoa uamuzi "haraka" juu ya jambo hilo, labda mwishoni mwa mwaka.