Mwanariadha wa zamani wa Olimpiki nchini Afrika Kusini Oscar Pistorius ameachiliwa huru kutoka jela siku ya Ijumaa, takriban miaka 11 baada ya kumuua kwa kumpiga risasi mpenzi wake Reeva Steenkamp.
Idara ya marekebisho ya Afrika Kusini imethibitisha kuachiliwa kwake siku ya Ijumaa asubuhi ikisema sasa, ''yuko nyumbani.''
Akiwa ametumikia zaidi ya nusu ya kifungo chake, mwanamichezo huyo mwenye umri wa miaka 37 hana viungo vya miguu yote miwili. Ataondoka katika gereza la Atteridgeville nje kidogo ya mji mkuu Pretoria.
Pistorius, anayejulikana ulimwenguni kote kama "Blade Runner" kwa sababu ya miguu yake ya bandia, hataruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari kama sharti la kuachiliwa kwake.
Rufaa kadhaa
Wakuu wa magereza waliwaonya waandishi wa habari kwamba hakutakuwa na fursa ya kumpiga picha.
Pistorius alimuua Steenkamp, mwanamitindo ambaye alikuwa na umri wa miaka 29 wakati huo, alfajiri ya Siku ya Wapendanao 2013, kwa kufyatua risasi nne kupitia mlango wa chooni wa nyumba yake ya Pretoria yenye ulinzi mkali.
Mauaji hayo yalifanyika mwaka mmoja baada ya Pistorius kuweka historia ya kuwa mchezaji wa kwanza mwenye miguu miwili bandia kukimbia katika kiwango cha Olimpiki alipotokea katika michezo ya London 2012.
Alipatikana na hatia ya mauaji na alihukumiwa kifungo cha miaka 13 jela mwaka wa 2017 baada ya kusikilizwa kwa muda mrefu na rufaa kadhaa.
Alikuwa amekana mashtaka na alikana kumuua Steenkamp kwa hasira, akisema alidhania alikuwa ni mwizi.
Mamake Steenkamp amesema hakuamini kwamba alikuwa amesema ukweli kuhusu kilichotokea.
Tiba kwa Pistorius
"Mtoto wangu mpendwa alipiga kelele kwa ajili ya maisha yake kwa sauti ya kutosha hadi majirani wamemsikia. Sijui ni nini kilimsababisha kuchagua kufyatua risasi kwenye mlango uliofungwa," June Steenkamp alisema katika wasilisho lake mahakamani.
Kwa kawaida, wahalifu nchini Afrika Kusini hustahiki kuzingatiwa kuachiliwa kwa masharti baada ya kutumikia nusu ya kifungo chao.
Pistorius alipoteza zabuni ya kwanza mwezi Machi wakati bodi iligundua kuwa hakuwa amekamilisha muda wa chini wa kizuizini unaohitajika kuachiliwa.
Mahakama ya Katiba mwezi Oktoba iliamua kwamba hilo lilikuwa kosa, na kuandaa njia ya kusikilizwa kwa kesi ya Novemba iliyoidhinisha kuachiliwa kwake.
Kama sehemu ya msamaha wake, hadi mwisho wa kifungo chake mnamo 2029, Pistorius lazima apate matibabu ya hasira na masuala ya unyanyasaji wa kijinsia.
Pia atapigwa marufuku kunywa pombe na vitu vyengine, akihitajika kukamilisha huduma ya jamii na pia kuwa nyumbani muda fulani wa siku.
Huku June Steenkamp hakupinga kuachiliwa kwa Pistorius na "aliridhishwa" na masharti hayo, hakushawishika kuwa amerekebishwa kikamilifu, msemaji wa familia amesema.
"Hakuna mtu anayeweza kudai kuwa na majuto ikiwa hawezi kujihusisha kikamilifu na ukweli," alisema katika taarifa.