Nyota wa soka wa Afrika Kusini Luke Fleurs ameuwawa katika tukio la uporaji gari, klabu yake ya Kaizer Chiefs imesema.
Mlinzi huyo mwenye miaka 24, alipigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa ni waporaji wa magari, katika tukio lililotokea katika kituo cha mafuta eneo la Honeydew, mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini.
"Luke Fleurs amefariki dunia katika tukio la uporaji mjini Johannesburg. Tunaungana na familia yake katika kipindi hiki kigumu," ilisema klabu ya Kaizer Chiefs kupitia taarifa yake.
Kwa mujibu wa msemaji wa Jeshi la Polisi la nchi hiyo Mavela Masondo, wauaji hao walitokomea na gari la Fleurs, mara baada ya kutekeleza mauaji hayo.
"Fleurs alikuwa anasubiri kuwekewa mafuta kabla ya kuvamiwa na watuhumiwa hao ambao walimpiga risasi kifuani huku mmoja akifanikiwa kukimbia na gari la mchezaji huyo," alisema Masondo.
Hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo hadi sasa, limesema jeshi hilo.
Jitihada za kumuwahisha hospitali hazikuzaa matunda kwani alipoteza uhai wake mara tu baada kufikishwa hospitali.
Mlinzi huyo wa kati alishiriki michuano ya Olimpiki ya mwaka 2021, na kuitwa katika timu ya taifa ya Bafana Bafana kwenye mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia, dhidi ya Ethiopia.
“Tumepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mchezaji huyo chipukizi. Ni pigo kubwa kwa familia yake, marafiki zake, wachezaji wenzake na familia nzima ya soka,” imesema taarifa ya Rais wa Chama cha Soka cha Afrika Kusini Danny Jordaan.