Rais William Ruto wa Kenya ametengua baraza la mawaziri nchini Kenya akisema  amezingatia maombi ya wananchi / picha kutoka Ikulu Kenya 

Na Coletta Wanjohi

Istanbul, Uturuki

Nchini Kenya, habari kubwa inayojadiliwa katika pembe zote za nchi ni kufutwa kazi kwa mawaziri wa nchi hiyo 11 Juni 2024.

Picha za mawaziri 22 pamoja na Mwanasheria Mkuu ziliondolewa mara moja katika tovuti ya serikali punde tu baada ya Rais kutangaza rasmi.

Rais Ruto amesema uamuzi wake kuvunja baraza lake la mawaziri unatokana na kuwasikiliza wananchi na kuangalia utendaji kazi wa mawaziri wake.

Kwa upande mmoja ni majonzi kwa mawaziri waliotimuliwa, kwa upande mwengine, ni furaha na vifijo kwa wananchi wanaomsifu rais kwa kuanza kuchukua hatua dhidi ya utawala mbovu.

Wataalamu wa kisiasa wanasema kuwa, huu ni wakati muafaka wa Rais Ruto kuunda serikali ya mawaziri wenye utaalamu zaidi katika sekta mbalimbali na sio kuteua kwa misingi ya kisiasa.

Hii ni mara ya pili katika historia ya Kenya kwa rais kuvunja baraza la mawaziri.

Novemba 23, 2005, aliyekuwa rais wa wakati huo Mwai Kibaki alivunja Baraza lake lote la Mawaziri, siku mbili tu baada ya rasimu ya katiba aliyoiunga mkono vikali kukataliwa katika kura ya maoni ya kitaifa.

Na kama ilivyo kwa Ruto, Kibaki pia hakugusa ofisi ya Makamu wake.

Wananchi hivi sasa hamu yao kubwa ni kuona muundo wa Baraza Jipya la Mawaziri.

Kulingana na katiba ya Kenya, Rais atapendekeza baadhi ya majina, na kwa idhini ya Bunge, atateua Makatibu wa Baraza la Mawaziri.

Kwa mujibu wa katiba ya Kenya, Katibu wa baraza hataruhusiwa kuwa mbunge pia.

Katiba inamruhusu rais kuteuwa hadi mawaziri 22 na idadi ya chini kabisa anayoweza kuchagua ni 14.

Wataalamu wanasema Rais Ruto huenda akawa amevuka kigingi kimoja, lakini sasa jukumu kubwa zaidi linamngoja, ni lile la kusuka upya safi ya viongozi wake watakaotimiza kiu cha wakenya.Wananchi wanafuatilia kwa karibu, ikiwemo kizazi cha Gen Z ambacho katika wiki kadhaa zilizopita, kiliingia mitaani na kushinikiza mabadiliko serikali.

TRT Afrika