Mzozo nchini Sudan uko katika siku yake ya sita huku kukiwa na usitishaji vita usio rasmi wa saa 24 kama ilivyotakiwa kukubaliwa na majenerali wawili wanaozozana nchini humo.
Hali bado haijulikani na risasi bado hazijasitishwa. Hali ni ngumu na yenye mambo mengi kutoka kwa watu wawili wakubwa waliohusika na simulizi iliyokabidhiwa kwa umma moja kwa moja kutoka kwa vyombo vya habari vya kimataifa.
Mambo kwa raia wa kawaida ni magumu zaidi.
TRT Afrika ilipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya watu mjini Khartoum na hadithi zao tangu machafuko ya Jumamosi yaanze.
Wengi wana hadithi za kusikitisha na ushuhuda ambao huleta picha na video halisi kueleza yale yanayosambazwa mtandaoni.
Siku ambayo mambo yote yalianza
Shakur Nya Keto, ni mkazi wa Khartoum, kutoka Khartoum Kusini, ambaye alikuwa akielekea kazini Jumamosi asubuhi kama ilivyo kawaida yake, alikuwa anaenda kushusha mzigo kukatokea ghafla mabadiliko kidogo katika mpango wake wa kawaida kwenye njia ya kuelekea kazini.
"Nilikuwa nikielekea kazini nikijua nina kazi ya kutoa, na wakati nikielekea huko, barabara ilifungwa na jeshi na katika dakika chache, nilisikia milio ya risasi."
Nya Keto anaeleza, "na hivyo nikaanza kukimblia nyumbani, Milio ya risasi ilipoanza, tulisikia sauti kubwa na nzito sana mshindo flani ... nilikimbilia nyumbani ili kuhakikisha kwamba watu katika familia yangu walikuwa salama."
Kaka yake alipigwa risasi na kupelekwa hospitali, hivyo alipokea simu akiwa nyumbani ikimfahamisha kilichotokea.
"Ilibidi nimtoe hospitalini kwani sikujua ni nani angedhibiti hospitali na ilibidi nimrudishe nyumbani, kumweka pale, tukimtibu peke yetu huku nikimsafisha majeraha, vidonda na kusimamisha uvujaji wa damu," Nya Keto anafafanua, “Ndugu yangu alipigwa risasi, nami nikachukua na kuitunza familia yake kwangu”
Zimesalia wiki kadhaa kabla ya mke wa Nya Keto kujifungua mtoto wao wa kwanza, na inaanza kuonekana kama mchakato huo utakuwa mgumu zaidi kama ilivyo kwa sababu madaktari wake hawapatikani.
Huku mahitaji zakizidi kuongezeka lakini upatikanaji kupungua ndani ya muda mfupi kama huu, wenyeji wanalazimika kuhatarisha maisha yao ili kupata chakula.
“Watu wanafungua maduka machache sana, na ni maduka madogo tu ndiyo yamefunguliwa kwa sasa, lakini maduka mengi ambayo yapo wazi, yanafunguliwa kwa masaa 2 au 3 na foleni ni ndefu. Lakini hata kufungua ni baada ya kuchungulia barabarani kuona pako salama."
Yusra Salih pia ni mkazi wa Khartoum kutoka Alazhari City; alitoka Misri usiku wa Ijumaa walipokuwa likizo na mumewe.
"Nilikuwa nikipanga kwenda ofisini Jumamosi asubuhi, na sikutarajia kungekuwa na vita hivyo, nilikuwa nimelala tu, na ghafla, asubuhi ya Jumamosi, niliamshwa na mlipuko wa bomu." Anaeleza Salih.
“Jambo la kwanza nililofanya ni kuwapigia simu familia yangu na kujua walikuwa wanaishi eneo tofauti na mimi. Nilijaribu kuwapigia simu ili kupata uhakika na usalama wao. Wako sawa? Je, wako mbali na mzozo, ili kujua mahali walipo, kumbe na wao walikua karibu na mapigano."
Wakwe wa Salih wanaishi Khartoum, na walikuwa wakimjulisha kuhusu kinachoendelea kwao, ambayo ni karibu sana na mapigano yanayoendelea.
Salih anakumbuka "hadithi za ajabu" kuhusu jeshi na shughuli za wanamgambo zilizoenezwa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Alhamisi ambazo hakuzichukulia kwa uzito, "Nilipata taarifa hizo kwenye Facebook, lakini sijui ni nani aliyeanzisha hadithi hizo wallahi!"
"Sijatoka nyumbani, natoka tu usiku kwa dakika chache kupata chakula, na sio asubuhi, sio mchana, usiku tu." Kwa hiyo kuanzia saa nane mchana, watu hutoka nyumbani ili kupata chakula kisha kurudi nyumbani. Huku ufyatuaji risasi na mabomu ukionekana kupungua usiku, lakini tunasikia risasi kila siku."
Maji na umeme zimekatwa
Leo, watu wengi mjini Khartoum hawana maji wala umeme. Wanapaswa kutegemea watu wanaoishi karibu na maeneo yaliyotengwa ya viwanda na matibabu kwa usambazaji wao duni wa rasilimali. Hata upatikanaji wa mtandao ni changamoto kwa wakazi.
Yusra Salih anaelezea jinsi wanafamilia wake wanavyokuja nyumbani kwake kila siku usiku kuchaji simu zao na kuoga.
"Hakujakuwa na umeme katika jiji, na kushangaa jinsi hii ilifanyika, lakini kila siku saa 2 usiku, watu hutoka nje ili kupata chakula na kama kuna giza kwani wanahisi salama zaidi."
Huku Khartoum ikipata halijoto ya hadi nyuzi joto 40, kukatika kwa umeme hufanya iwe vigumu kwa watu kufanya kazi bila maji na umeme.
"Watu huja na kuchaji simu zao na kuoga nyumbani kwetu. Nguzo kubwa yakusambaza umeme mjini kimekatwa, ila nashangaa bado tuna umeme na mawasiliano huku.” Nya Keto anaeleza.
Familia zinazohamia nje ya mji
"Nataka kuchukua familia yangu tutoke hapa ... Tumepoteza mawasiliano na familia na marafiki, hata huko Darfur, na hakuna njia ya kutoka Khartoum." Nya Keto aeleza.
"Tiketi ya nje ya mji imetoka dola 30 hadi 120 ili nifike Darfur. Kwa hivyo watu hawajui jinsi ya kutoka nje ya jiji wakati bei zinapanda kila kukicha."
Akiwa amejificha ndani ya nyumba pamoja na watoto wa kaka yake, mke wake na wapwa wawili, wanafunzi wa chuo kikuu, hakuna dalili wazi ya lini hii itaisha.
"Watu wa Sudan wanataka tu hii iishe! Usitishaji vita hautafanyika, kwa hivyo hakuna ratiba iliyo rasmi, kwa maoni yangu.
Yusra Salih anasema anahofia maisha yake.
“Nina hofu, na sina matumaini hata kidogo. Wataendelea mpaka lini? Wiki moja, wiki mbili au miezi? Na unajua hali ya uchumi ilivyo nchini Sudan, natumai kusitishwa kwa mapigano na kwamba waache kwa haraka iwezekanavyo! "