Mamlaka ya Nigeria ilisema operesheni ya kuwakamata wafungwa waliotoroka inaendelea. / Picha: Reuters

Mafuriko makubwa yaliporomosha kuta katika gereza moja huko Maiduguri kaskazini mashariki mwa Nigeria mapema wiki iliyopita, na kuruhusu wafungwa 281 kutoroka, wakuu wa magereza walisema Jumapili.

Wafungwa saba kati ya waliotoroka wamekamatwa tena katika operesheni na vyombo vya usalama, Umar Abubakar, msemaji wa Huduma za Urekebishaji Nigeria alisema katika taarifa.

"Mafuriko yalibomoa kuta za vituo vya kurekebisha tabia ikiwa ni pamoja na gereza la usalama wa kadri, pamoja na makao ya wafanyikazi jijini," Abubakar alisema.

Operesheni za kuwakamata wafungwa waliosalia zinaendelea, alisema.

Mafuriko mabaya zaidi

Maiduguri ni mji mkuu wa jimbo la Borno ambalo mapema juma lililopita lilikumbwa na mafuriko mabaya zaidi kuwahi kutokea katika miongo kadhaa.

Mafuriko hayo yalianza baada ya bwawa kufurika kufuatia mvua kubwa iliyonyesha na kuharibu mbuga ya wanyama inayomilikiwa na serikali na kuosha mamba na nyoka katika jamii zilizofurika.

Mafuriko hayo yamesababisha vifo vya takriban watu 30 kwa mujibu wa shirika la dharura la nchi hiyo na kuwaathiri wengine milioni moja, huku mamia ya maelfu ya watu wakilazimika kuingia katika kambi za watu waliokimbia makazi yao.

TRT Afrika