Amnesty International ilisema takriban watu 13 walikufa wakati wa mapigano na vikosi vya usalama katika siku ya kwanza ya maandamano.. Picha : Reuters

Nigeria iliwashtaki watu 76, wakiwemo watoto 30, kwa uhaini na kuchochea mapinduzi ya kijeshi baada ya kushiriki katika maandamano makubwa ya Agosti dhidi ya matatizo ya kiuchumi, nyaraka za mahakama zilionyesha siku ya Ijumaa.

Waandamanaji mwezi Agosti walifanya maandamano mjini Abuja, mji mkuu wa kibiashara wa Lagos na miji mingine kadhaa kuonyesha kutoridhika na mageuzi ya kiuchumi ambayo yamesababisha mfumuko wa bei uliokithiri na kusababisha matatizo yanayoongezeka kwa Wanigeria wa kawaida.

Rais Bola Tinubu ameapa kuendeleza mabadiliko ambayo anasema yanahitajika ili kuiweka nchi sawa.

Amnesty International ilisema takriban watu 13 walikufa wakati wa mapigano na vikosi vya usalama katika siku ya kwanza ya maandamano.

Shirika la kutetea haki za binadamu limesema watoto hao wameshikiliwa tangu mwezi Agosti na polisi wa Nigeria baada ya kushiriki katika maandamano ya kupinga kuzidi kukithiri kwa ukosefu wa usalama na kunyimwa haki nchini humo.

Hati ya mashtaka ilisema washukiwa hao walichunguzwa kati ya Julai na Agosti.

Kwa mujibu wa shirika la Reuters, juhudi za kupata jibu kutoka kwa msemaji wa polisi kuhusu kukamatwa kwa watoto hao hazikufua dafu.

Watoto hao walipewa dhamana na kesi hiyo itasikilizwa Januari, mawakili wao walisema.

Raia wa Nigeria wanakabiliana na mgogoro mkubwa wa gharama za maisha na ukosefu wa usalama ulioenea ambao umeharibu sekta ya kilimo, huku magenge yenye silaha yakiteka nyara wakazi na watoto wa shule kwa ajili ya fidia kaskazini.

Reuters