Baadhi ya raia wa Nigeria wametangaza nia yao ya kufanya maandamano siku ya Jumanne, Oktoba 1, wakati taifa hilo la Afrika Magharibi litakapokuwa likiadhimisha miaka 64 ya uhuru wake.
Waandalizi wa maandamano hayo wanasema maandamano hayo, yaliyopewa jina la #FearlessOctober1, yatafanyika kote nchini kushinikiza kurejeshwa kwa ruzuku ya mafuta, na pia kushughulikia maswala mengine ya umma.
Juwon Sanyaolu, mratibu wa kitaifa wa vuguvugu la vijana wa Nigeria, alisema Jumapili kwamba polisi wamefahamishwa kuhusu maandamano yaliyopangwa kama inavyotakiwa na sheria.
"Tumemwandikia inspekta mkuu wa polisi kumfahamisha kuhusu maeneo yetu ya maandamano," Sanyaolu alisema, kama alivyonukuliwa na gazeti la Punch la Nigeria.
Polisi washika doria
Waandalizi wa maandamano hayo wanasema yatakutana katika uwanja wa Eagle Square katika mji mkuu Abuja, na chini ya darajala Ikeja katika jiji la kibiashara la Lagos.
Inspekta Jenerali wa Polisi wa Nigeria Kayode Egbetokun ameamuru kutumwa kwa maafisa wa polisi katika vituo vya kimkakati vya serikali ili kuwalinda dhidi ya uharibifu unaowezekana.
Egbetokun pia amewataka wanaopanga maandamano hayo kubatilisha uamuzi wao.
Waandalizi wa maandamano hayo wanasema maombi yao ya awali kwa serikali kuhusu kupunguza matatizo ya kiuchumi hayakusikilizwa, na hivyo kusababisha wimbi jipya la hatua za mitaani.
Janga la gharama ya maisha
Kwa sasa Nigeria inapambana na janga la gharama ya maisha linalosababishwa na mfumuko wa bei, naira iliyoshuka thamani, na kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta.
Rais Bola Tinubu amewataka Wanigeria kuwa na subira na sera za kiuchumi za utawala wake akisema hivi karibuni zitazaa matunda.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, takriban Wanigeria milioni 25 wanakabiliwa na tisho la njaa.
Ukosefu wa usalama pia unasalia kuwa changamoto kubwa kwa serikali ya Rais Tinubu, huku utekaji nyara kwa ajili ya fidia na mashambulizi ya waasi yakiongezeka.
Maandamano hatari
Wakati wa maandamano ya hivi majuzi yaliyofanyika nchini Nigeria mapema mwezi Agosti, takriban watu 13 waliuawa. Amnesty International ilikadiria idadi ya waliofariki kuwa zaidi ya 21.
Mamia ya watu walikamatwa wakati wa maandamano hayo, huku wengi wao sasa wakikabiliwa na hatua za kisheria.