Idadi ya walioambukizwa na virusi vya Mpox nchini Nigeria yafikia hadi 48, huku virusi hivyo sasa vikiripotiwa katika mji mkuu Abuja na majimbo mengine 20, kulingana na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Nigeria (NCDC).
Licha ya kuongezeka kwa visa hivyo, hakuna vifo vilivyoripotiwa hadi sasa.
Serikali ilipokea shehena ya chanjo 10,000 kutoka Marekani mnamo Agosti 27 ili kusaidia kudhibiti mlipuko huo.
Zaidi ya hayo, fomu ya kujaza ufuatiliaji wa afya kwa wasafiri wa kimataifa imeanzishwa ili kusaidia kuzuia kuenea kwa virusi.
Umoja wa Afrika umetangaza dharura ya afya ya umma ili kukabiliana na kuenea kwa kasi kwa virusi katika bara zima.
Mpox huambukizwa kwa kugusana na mtu alioambukizwa, au vitu venye maambukizi.
Dalili huonekana siku 5 hadi 21 baada ya kuambukizwa na hujumuisha homa, maumivu ya mwili, uvimbe na vidonda vya ngozi.
Ingawa hakuna matibabu maalum, dawa za kuzuia virusi zinaweza kusaidia kudhibiti hali hiyo. Maambukizi mara nyingi huisha yenyewe, na alioambukizwa hupata afueni hutokea ndani ya wiki chache.
Mnamo 2022, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilibadilisha jina la "monkeypox" kuwa "mpox" ili kuondoa wasiwasi kuhusu ubaguzi wa rangi na ubaguzi unaohusishwa na neno hilo.