Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amehudhuria mkutano wa kikazi wa pamoja katika mji mkuu wa Niamey nchini Niger.
Alisafiri katika taifa hilo la Afrika Magharibi katika ziara rasmi ya siku moja.
Fidan ameandamana na Waziri wa Ulinzi Yasar Guler, Waziri wa Nishati na Maliasili Alparslan Bayraktar, Mkuu wa Ujasusi Ibrahim Kalin, Katibu wa Viwanda vya Ulinzi Haluk Gorgun, na Naibu Waziri wa Biashara Ozgur Volkan.
Kikao hicho kiliongozwa na Waziri Mkuu wa Niger Ali Mahamane Lamine Zeine siku ya Jumatano, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilisema kwenye mtandao wa X.
Duru za kidiplomasia siku ya Jumanne zilisema masuala yanaotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo, ni uhusiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili, matukio ya sasa hivi katika eneo la Sahel, na masuala ya kikanda, ikiwa ni pamoja na mzozo wa Israeli na Palestina.
Kuongezeka kwa hisia za dhidi ya Magharibi
Mwaka jana, wanajeshi nchini Niger walitangaza mapinduzi kupitia televisheni ya moja kwa moja, na kumtimua Rais Mohamed Bazoum, ambaye alijaribu bila mafanikio kupambana na shughuli za kigaidi nchini humo kwa msaada wa wanajeshi wa Ufaransa.
Zaidi ya hayo, kulikuwa na madai kwamba Rais Bazoum alikuwa akitumikia maslahi ya Ufaransa, na shutuma hizi zilitumika kuhalalisha kuondolewa kwake madarakani, zikiongozwa na Jenerali Abdourahmane Tchiani.
Kabla ya mapinduzi ya kijeshi, Niger ilikuwa mshirika muhimu wa kiuchumi na kiusalama kwa nchi za Magharibi katika eneo la Sahel.
Hata hivyo, junta iliyochukua udhibiti iliahidi kukata uhusiano na nchi za Magharibi, na kupitia upya mikataba ya madini na kuondolewa kwa askari wa Magharibi kutoka Niger.
Baada ya mapinduzi, wananchi wa Niger waliandamana na kuushambulia ubalozi wa Ufaransa. Kihistoria, baadhi ya malalamiko yao yanaweza kufuatiliwa hadi jinsi utawala wa kikoloni wa Ufaransa ulivyonyonya rasilimali na kutumia mbinu za kikatili za kidhalimu ili kujiendeleza.
Hata baada ya nchi za Kiafrika, kama vile Niger, kupata uhuru, Ufaransa iliendelea kuingilia siasa na uchumi wao.
Niger ilitangaza mwezi Machi kuwa inatengua makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi na Marekani, ikisema kuwepo kwa wanajeshi wa Marekani sasa ni "haramu".
Nchi hiyo imekuwa na makao makuu ya Marekani kwa kile kinachoitwa oparesheni za kukabiliana na ugaidi huko Afrika Magharibi, ikiwa na kituo kikubwa cha ndege zisizo na rubani za Marekani karibu na mji wa kaskazini wa Agadez ambao uligharimu dola milioni 100 kujenga.
Tangu mwaka wa 2019, jeshi la Marekani limetumia ndege zisizo na rubani na ndege za kijeshi kutekeleza misheni ya uchunguzi kutoka kambi ya jeshi la anga iliyoko nje kidogo ya Agadez. Ndege zisizo na rubani za jeshi la Marekani Reaper zimekuwa zikiruka hadi kwenye mipaka ya nchi jirani za Libya, Chad, Nigeria na Mali ambazo zina uwezo mdogo wa uchunguzi wa angani.