Ndege ya kijeshi iliyokuwa ikielekea kuwaokoa raia wa Uturuki kutoka eneo la machafuko nchini Sudan imeshambuliwa kwa risasi, imesema taarifa kutoka kwa Wizara ya Ulinzi ya Uturuki.
Ndege hiyo aina ya C-130 iliyokuwa ikielekea kambi ya kijeshi ya Wadi Seidna kwa shughuli ya uokoaji ilishambuliwa kwa kufyatuliwa risasi, kwa mujibu wa taarifa hiyo ya kijeshi iliyotolewa siku ya Ijumaa.
Hata hivyo ndege hiyo iliweza kutua salama na hakukuwa na majeruhi, taarifa hiyo iliongeza kusema.
Awali akizungumzia shughuli ya uokoaji inayoendelea, wizara hiyo ilisema: “ Kundi la kwanza la raia wetu lilirudishwa Uturuki kwa kutumia ndege zinazomilikiwa na jeshi la Uturuki”
Shughuli hiyo ya uokoaji itaendelea hadi raia wote wa Uturuki watakapo ondolewa nchini Sudan, Wizara iliongeza.