IMF Imeshutumiwa kuwekea mataifa ya Afrika masharti magumu katika kulipa madeni wanayopokea kutoka kwao Picha AA

Na Zanji Sinkala

Shirika la fedha duniani (IMF) limepata sifa mbaya katika miaka iliyopita katika ngazi mbali mbali kutokana na athari za sera zake za malipo ya deni wanazotoa kwa mataifa yanayostawi.

IMF imesema kuwa sera zake haziwezi kupuuza mahitaji ya wananchi, lakini je ndivyo hali ilivyo au ni porojo za kujisafisha?

Madeni ya kimataifa yamesakama nchi nyingi hasa mataifa yanayostawi katika miaka ya hivi karibuni wakati kumetokea majanga mabaya kama vile Uviko-19 na vita vya Ukraine.

Katika juhudi za kutaka kujikwamua kutoka kwa dhiki ya kiuchumi, mataifa mengi yamekimbilia mashirika ya kimataifa ya fedha kama vile IMF kwa kile wanachoita ‘ukombozi’ au ‘ruzuku ya deni’.

Hata hivyo gharama za madeni hayo zimewazidishia matatizo na kuzisukuma nchi ambazo tayari zinakumbwa na ugumu, katika madeni zaidi. Mojawapo ni Sri Lanka.

Taifa hilo limepata mkasa mbaya zaidi wa kiuchumi katika miaka 70 kufuatia kushindwa kwa mara ya kwanza katika historia kulipa deni hilo mnamo Mei 2022.

Zambia nayo pia sio geni katika suala la kushindwa kulipa madeni yake. Mwaka 2022 Zambia ilikuwa nchi ya kwanza ya Afrika kushindwa kulipa deni lake la nje la $17.3 bilioni za Marekani.

Baadhi ya masharti yanayotolewa na  IMF katika kutoa deni kwa wa Afrika yanahujumu maendeleo ya mataifa hayo Picha : AA

Wakati huo serikali ya rais Edgar Lungu iliiomba IMF kuikomboa huku ikitaja mkasa wa Uviko-19 kuwa sababu, pamoja na ukame uliotokea mwaka uliotangulia.

Mwaka 2021, serikali mpya ya rais Hakainde Hichilema alisaini mkataba wa deni la $1.3 bilion kutoka kwa IMF ambalo lilinuiwa kurekebisha mfumo wa kulipa madeni yasiyohimilika, kuimarisha uchumi wa taifa na ukuaji.

Ugumu wa kufanya mabadiliko

Lakini deni hilo, kama ilivyo ada, lilikuja na masharti makali ikiwemo kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya serikali, jambo lililopelekea kukatwa ruzuku ya serikali katika bei ya mafuta na kupunguza makadirio ya pato la serikali kutoka asili mia 6 hasi hadi asili mia tatu ya ziada kufikia 2025.

Hili lilitokea miaka minane baada ya shirika la kimataifa la fedha IMF kuishauri serikali ya Zambia kuendeleza viwango vya mishahara ya wafanyakazi wa umma kwa 35% ya fedha zinazokusanywa ndani ya nchi, katika muda maalum na isizidi 8% ya jumla ya pato la serikali.

Serikali ilikubaliana na masharti hayo kwa kupunguza mishahara kwa upande mmoja na kuongeza marupurupu ya juu kwa upande mwingine.

Rais Wa Zambia Hakainde Hichelema amefanya mazungumzo mengi na mashirika ya kimataifa ya fedha Picha AA

Matokeo yake yakawatumbukia nyongo na kulazimisha kuwekwa viwango vya mwisho vya mishahara, ambalo baadaye lilihujumu uwezo wa muungano wa walimu kupigania nyongeza ya mishahara na mazingira bora ya ajira.

Hii inatazamiwa kuwa ilienda kinyume na madhumuni ya kuwezesha kutolewa elimu bora kwa wote.

“Huo ulikuwa wakati walimu walilipwa mishahara duni kabisa. Kisha kukawekwa viwango vya mwisho vya mishahara, mambo yakawa magumu.’’ Anakumbuka mwalimu mmoja mjini Lusaka ambaye hakutaka tutaje jina lake.

‘’Raia wa Zambia wanalea familia kubwa, kwa hiyo ilikuwa vigumu sana kwetu kupokea mabadiliko hayo. Na si hivyo tu bali hata hamu ya kufanya kazi ilididimia,’’ aliambia TRT Afrika.

Mfuko wa machungu

Rueben Lifuka, mwanaharakati wa uongozi bora anasema kuwa shaka walionayo wananchi wa Zambia inatokana athari walizopata katika masharti ya kupata madeni ya IMF ya awali.

Serikali ya Zambia imezindua mradi wa CDF unaolenga kuwasaidia wananchi wa pato la chini Picha : Twitter HHichilema

Hata hiovyo amesema kuwa serikali ilitakiwa kuwa waangalifu zaidi katika kupokea madeni haya ya IMF na kuzingatia madhara yake kwa uchumi.

“IMF inapenda kusema kuwa hizi ni suluhisho za ndani kwa matatizo ya nchi. Wanadai kuwa serikali ya Zambia ndio iliyopanga kifurushi hiki. Lakini sisi tunakubali tu maneno hayo. Pengine tuulize swali moja au mawili lakini kwa kiasi kikubwa tunakubaliana nayo tu,’’ aliambia TRT Afrika.

‘’Idadi kubwa ya nchi zinakwenda kwa IMF wakiwa hoi kabisa, tayari wanapata tabu kiuchumi,” Lifuka ameelezea.

Mtetezi huyo wa utawala bora hata hivyo anasema kuwa serikali hizi zinalazimika kufanya mabadiliko yanayoishia kuwaathiri wananchi wao

Huku Zambia ikilenga mbele, wachambuzi wanasema kuwa ni muhimu sana kwa wanaounda sera kutafuta njia zinazofaidi pande zote katika mifumo ya kufufua uchumi huku wakiweka mbele zaidi maslahi ya wananchi wao na ukuaji wa uchumi unaohimilika.

TRT Afrika