Akizungumza kwenye kipindi cha JKLive Show cha Citizen TV Jumatano, Balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman ameonekana kutoridhishwa na mpango wa Rais William Ruto wa kuongeza kiwango cha ushuru wa Kenya kutoka asilimia 14 hadi 22 kufikia mwisho wa muhula wake. Huku akikubali mzigo wa kiuchumi ambao Wakenya watalazimika kubeba ili kufikia lengo hili, Ruto anaamini kwamba manufaa ya muda mrefu yatahalalisha ongezeko la ushuru.
"Suala la ushuru ni tatizo katika kila nchi na tunachosikia kutoka kampuni za Marekani ni kwamba Kenya inahitaji kutozwa ushuru wa chini lakini uwe thabiti; kuweka ushuru sawa kwa miaka mitatu, minne, au mitano kwa sababu wafanyabiashara hufanya uwekezaji kwa upeo wa faida," alisema.
Katika mahojiano yake Balozi huyo alipendekeza kupanuliwa wigo wa ushuru kupitia uundaji wa kazi badala ya kuongeza viwango vya ushuru.
"Kuna njia mbili; kuongeza kodi na pia kupanua wigo wa kodi ambayo ni idadi ya watu wanaotozwa ushuru na ndiyo maana ajira ni muhimu sana. Tengeneza ajira inayolipa vizuri, na malipo ya kudumu na baadhi ya marupurupu. Watu wengi wanapokuwa na mapato ya kutosha wanaweza kulipa kodi, kwa hivyo upanue idadi ya watu na sio kutoza ushuru watu hao hao kila siku," alisema Balozi Whitman.
Upandishaji wa ushuru
Hapo awali, Rais Ruto ametetea mpango wa serikali yake wa kutoza ushuru wa ziada kwa Wakenya, akisema kuwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha mapato ya nchi na kupunguza utegemezi wa kukopa.
Ruto amefichua azma yake ya kuongeza kiwango cha ushuru nchini kutoka asilimia 14 ya sasa hadi asilimia 16 ifikapo mwisho wa mwaka huu na pia analenga kupandisha kiwango hicho hadi asilimia 22 ifikapo mwisho wa muda wake wa uongozi.
Huku akikubali mzigo wa kiuchumi ambao Wakenya watalazimika kuubeba ili kufikia lengo hili. Ruto anaamini kwamba manufaa ya muda mrefu yatahalalisha ongezeko la ushuru.
"Dhamira yangu ni kuisukuma Kenya, ikiwezekana mwaka huu tutaongeza ushuru hadi 16% kutoka 14%. Nataka katika muda wangu, Mungu akipenda, niiache kati ya 20 na 22%. Itakuwa ngumu, nina mambo mengi ya kuelezea, watu watalalamika lakini najua hatimaye watashukuru kwamba pesa tunazoenda kukopa kutoka Benki ya Dunia ni akiba kutoka nchi nyengine,” Ruto alisema.