Namibia ina jumla ya wapiga kura milioni 1.45 waliotimiza masharti ya kupiga kura ambao watamchagua rais na wajumbe wa Bunge la Kitaifa.  / Picha: AFP

Tume ya uchaguzi nchini Namibia imetangaza kuongeza siku mbili zaidi za kupiga kura katika baadhi ya vituo vya kupigia kura baada ya baadhi ya vifaa kuwa na hitilafu hivyo kuwazuia watu wengi kupiga kura Jumatano.

Jumla ya vituo 36 vya kupigia kura vitafunguliwa siku ya Ijumaa na Jumamosi, imesema Tume ya Uchaguzi ya Namibia, huku ikikiri kutokea kwa hitilafu za kiufundi katika baadhi ya vifaa hivyo kuchelewesha upigaji kura siku ya Jumatano na kuwaacha watu wakiwa kwenye foleni kwa zaidi ya saa 12.

Upinzani nchini Namibia ulikuwa umetoa wito wa kuongezwa kwa muda wa upigaji kura na kuhesabu kura, baada ya uchaguzi wa rais na wabunge kuvurugwa na ucheleweshaji mkubwa.

Wananchi wa Namibia wanapiga kura kumchagua rais mpya na wabunge katika uchaguzi ambao umehusisha vyama 14 vya kisiasa kikiwemo chama tawala cha SWAPO ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 34.

Baadhi ya wapiga kura milioni 1.45 waliotimiza masharti ya kupiga kura watamchagua rais na wajumbe wa Bunge la Kitaifa.

TRT Afrika