Namibia inajiandaa kwenda uchaguzi baadaye mwkaa huu ambapo chama tawala kinampendekeza  Netumbo Nandi-Ndaitwah, mwanamke wa kwanza kuwania kiti hicho / Picha : Reuters 

Nangolo Mbumba wa Namibia, ambaye alichukua wadhifa wa rais wa muda wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika siku ya Jumapili baada ya Hage Geingob kufariki akiwa madarakani, alisema hana mpango wa kugombea katika uchaguzi unaotarajiwa mwishoni mwa mwaka huu.

Hiyo ina maana kwamba Netumbo Nandi-Ndaitwah, ambaye anachukua nafasi ya Mbumba kama makamu wa rais na kupendekezwa na Chama tawala cha Umoja wa Watu wa Afrika Kusini Magharibi (SWAPO) zaidi ya mwaka mmoja uliopita kuwa mgombea wake, atasalia kwenye kura.

Iwapo atashinda, atakuwa rais wa kwanza mwanamke katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.

"Sitakuwepo kwa ajili ya uchaguzi kwa hivyo msiwe na hofu," Mbumba alisema katika hatua ambayo ni nadra miongoni mwa viongozi wa Afrika ambao mara nyingi wamekuwa wakitafuta kuhifadhi madaraka mara yanapokuwa mikononi mwao.

"Lengo langu lilikuwa kuwa mkuu wa shule, jambo ambalo nililifanikisha na sasa sina budi kuwashukuru watu wa Namibia kwa heshima waliyonipa ya kuwa rais wao, kwa kipindi kifupi," Mbumba alisema katika hafla ya kuapishwa kwake.

Katiba ya SWAPO, chama kinachotawala, inakataza kufanya mabadiliko mara mgombea anapochaguliwa miaka miwili kabla ya uchaguzi kukamilika.

Chama hicho kimeitawala Namibia - nchi iliyo na madini ya almasi, uranium na pia lithiamu inayohitajika kwa betri za magari ya umeme - tangu uhuru kutoka Afrika Kusini mwaka 1990.

"Inatia jambo la kuhuzunisha lakini pia kutia moyo kuona kwamba leo hii, hata katika wakati huu wa hasara kubwa, taifa letu bado limetulia," alisema Mbumba. "Hii ni kutokana na uongozi wenye maono wa rais Geingob ambaye alikuwa mbunifu mkuu wa katiba ya Namibia." aliongezea.

TRT Afrika