Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Namibia limetoa idhini kwa Wizara ya Masuala ya Ndani ya Nchi, Uhamiaji, na Usalama kuwasilisha mahitaji ya viza ya kuingia kwa nchi ambazo pia huwataka wananchi wa Namibia viza.
Hii inamaanisha kuwa raia wa nchi ambao walikuwa tu wanaingia nchini humo bila viza sasa watalazimika kuomba viza.
"Katika miaka ya hivi karibuni, Jamhuri ya Namibia kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Uhamiaji, na Usalama imeendeleza ishara za nia njema na upendeleo kwa raia wa nchi mbalimbali," imesema serikali ya Namibia.
Taarifa ya serikali imesema, licha ya jitihada hizo, baadhi ya mataifa hayajaridhia.
Namibia ni nchi kubwa kijiografia yenye idadi ndogo ya watu wapatao takriban milioni 3 na ukanda wa pwani wenye urefu wa kilomita 1,500 kwenye Atlantiki ya Kusini.
Ikiwa ni nchi kame zaidi katika Kusini mwa Afrika mwa Jangwa la Sahara, ina utajiri mkubwa wa rasilimali za madini, ikiwa ni pamoja na almasi na urani, ikigawana mipaka na Angola, Botswana, Afrika Kusini na Zambia.
Uamuzi huu ambao serikali ya Namibia imeutoa una nia ya kuimarisha usawa wa kidiplomasia na utaathiri nchi 31.
"Kwa kuzingatia tofauti hii, serikali imeona ni muhimu kutekeleza hitaji la viza ili kuhakikisha usawa katika kidiplomasia," imesema.
Ubelgiji, Uingereza, Canada, Ujerumani, Ureno ( Portugal), Uhispania, Italy, Uholanzi, Marekani na Japan zimetajwa katika orodha hiyo ya nchi 31.
"Wananchi wa nchi hizi 31 watapewa viza wakifika Namibia kwa kiwango fulani cha pesa, na baada ya maombi yao kuzingatiwa," Wizara ya Masuala ya Ndani ya nchi imesema.