Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Sudan Abdel Fattah Al-Burhan: Picha Reuters

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Sudan Abdel Fattah Al-Burhan amefanya mabadiliko kwenye baraza la mawaziri, huku vyombo vya habari vya Sudan vikisema uteuzi huo umewaondoa mawaziri watano.

Miongoni mwa walioteuliwa ni pamoja na Dr. Mohieddin Naeem Muhammad Saeed Bamaham, kuwa waziri mpya wa Nishati na Mafuta na kuchukua nafasi ya Mohamed Abdallah Mahmoud.

Wakati huo huo, Amal Saleh Saad ameachwa pembeni na kumteua Al-Fateh Abdullah Youssef, kuwa Waziri mpya wa Biashara na Ugavi.

Aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Hisham Ahmed Ali Abu Zaid ameachishwa kazi huku Abu Bakr Abu Al-Qasim Abdullah, akiteuliwa kuwa waziri mpya wa uchukuzi.

Ahmed Ali Abdel Rahman ametangazwa kuwa Waziri wa Kazi na Mageuzi ya Utawala.

Mbali na kuwateua mawaziri wapya, Jenerali Al-Burhan amemuondoa Waziri wa Mifugo Abdel Hafiz Abdel Nabi.

Mabadiliko haya ya Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Sudan Abdel Fattah Al-Burhan yanajiri huku pande zinazozana Sudan zikikutana kwa mazungumzo nchini Saudi Arabia.

TRT Afrika