Msanii wa Nigeria Samuel Perry alishinda tuzo ya muigizaji bora wa vichekesho kwa upande wa wanaume, kwa mwaka 2023. Picha : Samuel Perry/Instagram

Na Charles Mgbolu

Waandaaji wa tuzo za Africa Magic Viewers Choice Awards (AMVCA), wamewataka wasanii na watengeneza maudhui mitandaoni kuwasilisha kazi zao, huku kukiwa na mabadiliko makubwa kwenye mpangilio wa tuzo hizo zitakazofanyika mwezi Mei, 2024.

‘’Ni wakati muafaka, tunapoadhimisha miaka 10 ya tuzo hizi, kujitafakari na kupitia upya vipengele vya tuzo hizo ili ziweze kurandana na viwango vya kimataifa,'' alisema Busola Tejumola, mkuu wa maudhui na vipindi wa kampuni ya MultiChoice, kwa ukanda wa Afrika Magharibi.

''Hii itahusisha kuondoa baadhi ya vipengele, kuboresha vile vitakavyobaki na pia kupitia upya namna ya upigaji kura kwa washiriki,’’ aliongeza.

Kulingana na Tejumola, tuzo za mwaka huu zimeboreshwa zaidi kwani zitakuwa na vipengele vya Muigizaji Bora wa kike na wa kiume, katika nafasi za uongozaji na usaidizi, huku washindi wakiamuliwa na majaji, tofauti na utaratibu wa awali ambao kura za wazi kutoka kwa hadhira.

Tobi Bakre (watatu kutoka kushoto) alishinda tuzo ya mugizaji bora wa filamu kwa mwaka 2023./Picha: Wengine

Mabadiliko hayo yameibua hisia za furaha na matumaini kutoka kwa wafuatiliaji na wakosoaji tofauti wa tuzo hizo.

Upinzani mkali

Tuzo hizo ziliingia dosari mwaka jana, na kukosolewa vikali kwenye mitandao ya kijamii baada ya washindi kutangazwa.

Wakosoaji na wadau wengine wa burudani wameshauri kuondolewa kwa kura ya wazi wakati wa kumchagua muigizaji bora, kwani wale wenye ufuasi mkubwa kwenye mitandao ya jamii, huwa na nafasi kubwa ya kushinda kuliko wale wenye vipaji halisi vya uigizaji.

Hata hivyo, gumzo kubwa liliibuka baada ya jina la muigizaji kutoka Nigeria Kunle Remi kuondolewa kwenye orodha ya wateule wa tuzo hizo, licha ya nafasi yake aliyocheza kwenye tamthiliya ya Kunle Afolayan iitwayo Anikukapo ambayo ilipigiwa kura mara 16 katika tuzo hizo kubwa barani Afrika.

Kunle Remi alipata sifa nyingi baada ya kushiriki kwenye filamu ya Anikulapo./Picha: Kunle Remi Instagram

Kwa upande wake, Kunle alisisitiza kuwa hatua ya kuondoa jina lake kwenye orodha hiyo haikuwa na athari yoyote kwenye mtindo wake wa maisha na umaarufu wake.

Tuzo adilifu

‘’Hili si onesho langu japo najisikia faraja kuona watu wakitoa hisia zao, sifanyi kazi kwa ajili ya kupata tuzo lakini ni kwa nia ya kujipa changamoto siku hadi siku,’’ alisema.

Ingawa AMVCA haikujibu hoja hizo, mabadiliko haya mapya bado yanalenga kulinda hadhi za tuzo hizo barani Afrika.

‘’AMVCA itaendelea kuthamini utajiri wa vipaji vya wasanii katika tasnia ya tamthiliya barani Africa,’’ alisema Tejumola, kupitia picha mjongeo.

AMVCA imeendelea kusisitiza kuwa majaji wa mwaka huu watajumuisha nguli wa kutengeneza filamu na tamthiliya barani Afrika, japo majina yao bado hajawekwa wazi.

TRT Afrika