AMVCA 2023: Tuzo kubwa zaidi za filamu Afrika, faida kwa filamu za Kiswahili?

AMVCA 2023: Tuzo kubwa zaidi za filamu Afrika, faida kwa filamu za Kiswahili?

Tuzo hizo ni hafla ya kila mwaka inayowaheshimu watengenezaji sinema na waigizaji katika bara zima
Washindi wa vipengele thelathini na tatu vya tuzo watatangazwa ikiwa ni pamoja na tuzo za watu mashuhuri wa mitindo. Peter Kamau, Chris Atoh, Tobi Bakre, Stan Nze/ Istagram

Toleo la tisa la sherehe za tuzo za filamu maarufu barani Afrika, Africa Magic Viewers’ Choice Awards (AMVCA) zitafanyika Jumamosi hii Mei 20 jijini Lagos, Nigeria.

Tukio hilo litaanza na msururu wa shughuli za kabla ya onyesho huku sherehe kuu ya hafla itakuwa Jumamosi.

Katika taarifa yake kabla ya tukio hilo, Mkuu Mtendaji wa Idhaa za Maudhui na Chaneli za Afrika Magharibi, MultiChoice Nigeria, Busola Tejumola, alibainisha kuwa mwaka huu, tuzo za AMVCA zitapamba moto.

“Mwaka jana, tulikuwa na msururu wa shughuli za siku nane kuelekea usiku wa tuzo. Mwaka huu hautakuwa tofauti. Tumeamua kuendeleza kasi kwa kurudisha shughuli zote. Tofauti pekee ni kwamba yote yatafanyika ndani ya siku tatu”, ilisomeka taarifa hiyo.

Siku ya kwanza itaanza na tukio la kitamaduni na mnamo Ijumaa tarehe 19, baadhi ya wabunifu wa mitindo waliochaguliwa mapema watashindana katika pambano la ubunifu wa mitindo katika fashion show.

Usiku wa tuzo siku ya Jumamosi ndio kilele; itaadhimisha mwaka thabiti wa matoleo ya kipekee ya filamu na tamthilia kutoka kwa baadhi ya watengenezaji bora zaidi barani.

Femi Odugbemi, Mtayarishaji Mashuhuri wa filamu kutoka Nigeria, mtayarishaji na mwandishi, ndiye atakuwa jaji mkuu kwenye jopo la tuzo. "Tasnia ya filamu ya Kiafrika inakua na ina mabawa, hatuwezi kusubiri kuona itaishaje kwani ni ya kipekee na hadithi ni zetu wenyewe." akiongea na TRT Afrika Odugbemi aeleza kwa kusisitiza, akiongeza kuwa "watengenezaji filamu wa Kiafrika hawapaswi kufanya kazi dhidi yao au kushindana kwani wanapaswa kujinyanyua."

Hakika jambo moja juu ya yote ni kwamba uzalishaji wa filamu na tamthilia za Kiswahili zitaenea mbali kutokana na tuzo hizi.

Baadhi ya wateuzi katika Afrika Mashariki kwa lugha ya Kiswahili

Mzalishaji wa filamu na vipindi vya TV kutoka Tanzania, na teule wa mara ya kwanza kwenye soko, Wilson Nkya, ameteuliwa kupata nafasi ya kushinda katika vipengele viwili vya Filamu Bora Afrika Mashariki na Filamu Bora ya lugha ya Kiswahili kwa kutengeneza filamu ya Frida na Mvamizi.

"Inanitia hamasa sana na imekuwa kama siamini kwamba naweza kupata heshima na nafasi hii kuaminiwa sasa zinanitambulisha katika tuzo kubwa kama hizi." Mchipukizi Nkya asema akiongeza kwamba ni mara yake ya kwanza kuteuliwa.

"Kasi ya filamu ni ndogo kwa sababu sekta ya filamu miaka ya nyuma ilikuwa haija rasimishwa kwa hio ikawa haichukuliwi kwa uzito na uwekezaji ulikuwa mdogo mno, lakini sasa kuna channel zimetengenezwa kwa ajili ya kuendeleza filamu. Serikali sasa inatambua sekta na kuona umuhimu wake."

Nkya alitaja filamu kama iliyoingizwa katika tuzo za Oscars, Vuta Nkuvute (Tug of War) ya Amil Shivji na filamu ya Netflix ya Binti ya Seko Shamte, kama mifano ya mafanikio ya sekta ya Tanzania, japo kwa kasi ndogo.

Kwa kuwepo kwa tamasha kama vile Tamasha la Filamu la Zanzibar, ZIFF, nchini Tanzania kuna nafasi zaidi kwa filamu za Kiswahili kuenea mbali zaidi duniani kama hizo filamu "zitakuwa zinateuliwa kwa wingi zaidi".

Idris Sultan kutoka Tanzania pia amesimama kidete katika kitengo cha Filamu Bora Afrika Mashariki, akiwa kama mwandishi katika filamu ya vichekesho vya kimapenzi - Married to Work.

Sultan ameiambia TRT Afrika kuwa "Washinde au wasishinde katika tuzo za AMVCA, muhimu zaidi ni kwamba wameteuliwa na hio tayari ni ushindi tosha mpaka kufika huko".

"Married to Work ilikuwa namba 5 kwa Nigeria na namba 2 Kenya kwa filamu za Kiafrika kwa hiyo kama unavyoona ni kitu kizuri na kikubwa kama tunaweza eneza lugha." Sultan aliongeza.

Tasnia ya filamu nchini Kenya inasherehekea idadi kubwa zaidi ya walioteuliwa hadi sasa katika onyesho hili la kipekee, kwa jumla ya uteuzi 17.

Njoki Muhoho, ni Mtayarishaji Mtendaji wa kipindi cha Salem, ambayo pia imeteuliwa kwenye kipengele cha Tamthilia Bora Afrika, anaiambia TRT Afrika kuwa "unakosa pale ambapo hujaribu lakini unapojaribu unafanikiwa."

"watu wengi zaidi wanahitaji kuwasilisha filamu zao bila kuwa na wasiwasi kuhusu kama wewe utashinda au la maana hii ndio njia ya kuwa na uzalishaji mwingi zaidi kutangaza sanaa kutoka kanda letu."

Muhoho anaongeza kuwa ni muhimu kuwa wakweli na wa kiasili ikija kwenye kuzalisha maudhui yako, watu kutoka nchi yako watataka kuangalia "watu waliyofanana nao na wanaoishi maisha kama ya kwao."

Mwigizaji wa Uganda na mteule wa ‘Muigizaji bora wa Kiume katika filamu’ Patriq Nkakalukanyi amesifiwa kwa tafsiri yake nzuri katika filamu ya afya ya akili Tembele.

Mtanzania mwingine, na mshindi wa tuzo kama Mwendeshaji wa filamu, Daniel Manege, ameteuliwa na filamu yake ya Mpiganaji kupata nafasi ya kushinda tuzo chini ya kitengo cha filamu/mfululizo bora wa Lugha za Asili.

Zaidi ya wageni 3000 walihudhuria toleo la 8 la sherehe ya tuzo za AMVCA, / Picha: Roselyn Ngissa, Grace Wacuka, Erica Nlewedim, Osas Ighodaro / Instagram

Hakika kutakuwa ni mkusanyiko mkubwa wa wanafilamu bora zaidi wa Kiafrika katika tuzo za AMVCA ambao wamefanikiwa kusafirisha utamaduni wa filamu wa Kiafrika kwa ulimwengu mzima.

TRT Afrika