Serikali ya sasa ya Afrika Kusini imeundwa na vyama 10 vya kisiasa baada ya chama cha African National Congress (ANC) kukosa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura katika uchaguzi mkuu wa 29 Juni 2024.
Na huku harakati ya kujipanga kuunda serikali zikiendelea, chama cha African National Congress (ANC) kimeonyesha wasiwasi kuwa baadhi ya vyama vimekuwa vikitoa matakwa ya ajabu.
"Baadhi ya vyama vimekuwa vikitoa matakwa ya ajabu na ya kuudhi kwa nyadhifa maalumu za Baraza la Mawaziri kwenye vyombo vya habari," Fikile Mbalula katibu mkuu wa ANC amesema katika akaunti ya chama ya X.
Kiongozi wa chama cha DA John Steenhuisen amekashifiwa na ANC ambayo inadai kuwa katika barua aliyoandika anadai nyadhifa mbili za ziada katika baraza la mawaziri.
ANC inaikashifu DA kwa kutaka kuunda serikali nyengine kando na kufanya kazi nje ya vigezo vya kikatiba.
"Kujadiliana kupitia madai ya kuvujisha kwa vyombo vya habari ni kitendo cha nia mbaya na tabia hii haitasaidia sababu ya chama chochote. Ni Rais pekee ndiye mwenye maamuzi ya mwisho kuhusu uteuzi wa Baraza lake la Mawaziri," ameongezea.
Vyama 10 vya kisiasa ambavyo vimeunda serikali na ANC ni pamoja na Democratic Alliance DA ambayo ilikuwa ya pili kwa wingi wa kura katika uchaguzi mkuu.
Chama cha ANC kinasema Rais atatangaza baraza la mawaziri katika siku chache zijazo akizingatia katiba ambayo inampa kipaumbela kuteuwa mawaziri. Kwa sasa maongezi yanaendela kati ya ANC na vyama husika kuhusu suala hili .