Takriban watu 21, wengi wao wakiwa watoto, waliuawa siku ya Ijumaa wakati shule ilipoporomoka katikati mwa jiji la Nigeria la Jos, afisa wa Msalaba Mwekundu aliiambia TRT Afrika.
Baadhi ya wengine 71 walikuwa wakipokea matibabu katika hospitali kutokana na majeraha ya viwango tofauti, Nurudeen Hussaini Magaji, ambaye ni katibu wa Msalaba Mwekundu katika jimbo la Plateau, alisema.
Wengi wa wale waliokuwa katika jengo la ghorofa hilo la makazi ya Saints Academy katika mji mkuu wa Jimbo la Plateau walitoroka bila kujeruhiwa, aliongeza.
‘’ Wengi wa waathiriwa walikuwa na umri wa kati ya miaka 10 na 13,’’ Magaji aliongeza.
Alitaja tukio hilo kuwa ‘’ la kushtua na kuogopesha’’. Chanzo hasa cha kuporomoka kwa jengo hilo hakijafahamika hadi sasa, lakini tukio hili limetokea baada ya ‘’siku za mvua kubwa’’ jijini humo, alieleza.
Tukio baya la kusikitisha
Waathiriwa walipelekwa angalau katika hospitali tatu jijini, wakaazi walisema.
Baadhi ya waliojeruhiwa wanaripotiwa kuwa katika hali mbaya.
''Hali ni mbaya na ya kusikitisha. Nilienda katika hospitali mbili ambapo niliona maiti 16 zikiwa zimehifadhiwa kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti na pia baadhi ya wanafunzi waliojeruhiwa,'' aliyeshuhudia, Muhammad Shitu, aliiambia TRT Afrika.
''Miili yote niliyoiona ilikuwa ya wanafunzi. Hali ni mbaya sana. Walionusurika wamepoteza damu nyingi, na watu wanakimbilia kutoa damu,'' Shitu aliongeza.
Wanafunzi waliobaki chini ya vifusi walisikika wakilia kuomba msaada chini baada ya shule ya Saints Academy kuwaangukia wanafunzi hao.
Wachimba mitambo walijaribu kuwaokoa waathiriwa huku wazazi wakiwatafuta watoto wao.
Shughuli za uokoaji zaendelea
Akiwa na mama yake kando ya kitanda cha hospitali, mwanafunzi aliyejeruhiwa Wulliya Ibrahim aliiambia AFP: "Niliingia darasani si zaidi ya dakika tano, niliposikia sauti, na kilichofuata ni kujipata hapa." "Sisi ni wengi darasani, tulikuwa tunaandika mitihani yetu," alisema. Shirika la Kitaifa la Usimamizi wa Dharura lilisema jengo hilo liliporomoka na kuua "wanafunzi kadhaa" bila kutoa maelezo. "NEMA na wadau wengine muhimu kwa sasa wanafanya shughuli za Utafutaji na Uokoaji," ilisema. Mkazi katika eneo la tukio Chika Obioha aliiambia AFP aliona takriban miili minane kwenye eneo hilo na kwamba makumi ya wengine walikuwa wamejeruhiwa.
"Kila mtu anasaidia kuona ikiwa tunaweza kuokoa watu zaidi," alisema. Kuporomoka kwa majengo ni jambo la kawaida katika taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika kwa sababu ya uzembe wa utekelezaji na kutumika kwa vifaa vya ubora wa chini.
Ukarabati duni
Takriban watu 45 waliuawa mwaka wa 2021 wakati jengo refu lililokuwa likijengwa liliporomoka katika wilaya ya Ikoyi katika mji mkuu wa kiuchumi wa Nigeria Lagos.
Watu kumi waliuawa wakati jengo la ghorofa tatu lilipoporomoka katika eneo la Ebute-Metta mjini Lagos mwaka uliofuata.
Tangu mwaka 2005, angalau majengo 152 yameporomoka mjini Lagos, kulingana na mtafiti wa chuo kikuu cha Afrika Kusini anayechunguza majanga ya ujenzi.
Uundaji mbaya, vifaa vya ubora wa chini na ufisadi wa kupitisha uangalizi rasmi mara nyingi hulaumiwa kwa majanga ya ujenzi Nigeria.