Serikali ya Uingereza inataka kuwahamisha nchini Rwanda maelfu ya waomba hifadhi wanaofika Uingereza. / Picha: AFP

Kupitishwa kwa mswada tata wa Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak wa kuwapeleka wakimbizi nchini Rwanda huenda ukacheleweshwa hadi angalau mwezi ujao baada ya Baraza la Juu la Bunge la Uingereza kutaka maboresho zaidi kufanyika katika sheria.

Serikali inataka kuwahamisha nchini Rwanda maelfu ya waomba hifadhi wanaofika Uingereza kwa kutumia usafiri wa boti ndogo kila mwaka, lakini changamoto za kisheria zimezuia wahamiaji hao kupelekwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Sheria hiyo ni msingi wa ahadi ya Sunak ya kukomesha wimbi la wahamiaji wanaowasili na kutafuta hifadhi. Sunak amekuwa akiivalia njuga hatua hiyo kama sehemu ya kampeni ya chama chake cha Conservative, katika uchaguzi mkuu ujao.

Wajumbe wasiochaguliwa wa Baraza la Juu, wengi wao wakiwa wanasiasa wa zamani na maafisa wa serikali, walipiga kura Jumatano kwa mara ya pili kurekebisha sheria ili kuweka ulinzi zaidi wa haki za wanaotafuta hifadhi.

Wabunge hao walipigia kura marekebisho ambayo yangehitaji mawaziri kuzingatia "sheria za ndani na kimataifa" na zile ambazo lingetangaza tu Rwanda kuwa nchi salama wakati wa utekelezaji wa mkataba wa Uingereza.

Kushindwa kwa serikali kunamaanisha kuwa mswada huo utarejeshwa katika Baraza la Bunge katika mchakato unaojulikana kama "ping-pong ya bunge" ambapo mabunge hayo mawili yanajaribu kutafuta muafaka.

Hii inamaanisha kuwa, muswada huo hauwezekani kuwa sheria hadi baada ya bunge kurudi kutoka mapumziko yake ya Pasaka - katikati ya mwezi ujao.

Hili huenda ikarudisha nyuma mchakato huo wa kuwahamisha waomba hifadhi hao baada ya afisa mmoja wa serikali kusema kuwa huenda ikachukua angalau mwezi mmoja wa utekelezaji baada ya sheria kupitishwa.

TRT Afrika