Na Nadim Siraj
Mwanasheria mkuu wa zamani wa Marekani Ramsey Clark aliwahi kutoa uchunguzi kuhusu nafasi ya Marekani katika siasa za ulimwengu inayoitwa: “The greatest crime since World War II has been US foreign policy.”
Uchungunuzi huo unalingana na sura ya ulimwengu ulivyo sasa na kuendana na njama potofu ya Donald Trump ya kunyakua Gaza.
Rais huyo wa Marekani asiyetabirika alipita mpaka wakati hivi karibuni alipozindua mpango ambao ulivunja mipaka yote ya diplomasia.
Alipendekeza Marekani ichukue udhibiti wa Gaza iliyoharibiwa na vita, kuwaelekeza Wapalestina milioni 2.1 nje, na kuiendeleza kuwa "Riviera ya Mashariki ya Kati".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na katibu wa waandishi wa habari wa Ikulu ya Marekani Karoline Leavitt walifanya juhudi za kuzima moto kwa kuhakikisha kuwa huo ni mpango wa muda.
Lakini rais wao, alisisitiza tena kwamba Marekani "itachukua udhibiti wa Gaza" kwa hakika. "Tutaichukua, tutaishikilia, tutaithamini," aliwaambia waandishi wa habari katika Ofisi ya Oval.
‘Jambo la kushtua’, ‘kustaajabisha’, ‘isiyotarajiwa’, ‘isiyo na mfano’ - haya ndiyo baadhi ya maneno ni baadhi yanayotumiwa katika mijadala kuelezea mpango usiotekelezeka wa Trump.
Lakini mtu akichukua hatua kadhaa nyuma na kuangalia picha kubwa zaidi, mpango wa Gaza hauonekani kuwa wa kushangaza.
Si mpango wa ajabu
Kwa kweli, uchunguzi wa karibu wa historia ndefu na ya kutatanisha ya sera ya kigeni ya Marekani inaonyesha kinyume chake - kwamba mpango wa Trump kuhusu Gaza kwa hakika ni muendelezo wa ajenda ya muda mrefu ya Marekani ya uingiliaji wa masuala ya nchi zingine na upanuzi.
Gaza ni njama ya nyongeza tu katika misheni ya kibeberu ya kudumu ya Marekani ya uingliaji, uvamiaji, upigaji vita, na unyakuaji wa maeneo kwa ukiukaji wa sera za kidiplomasia.
Kumbuka kwamba wakati wa maandalizi ya kampeni ya urais ya Trump na ushindi wake wa baadae katika uchaguzi, Gaza haikuwa shabaha pekee.
Alikuwa akipiga kelele kwamba alitaka Marekani kuchukua udhibiti au kununua Kanada na Greenland, na kuchukua udhibiti Mfereji wa Panama.
Hata majina ya ghuba sio salama kutokana na ushawishi wa kijiografia wa Trump. Ikulu ya White House hivi majuzi ilifanya Ramani za Google ibadilishe jina la Ghuba ya Mexico kuwa 'Ghuba ya Marekani' kwa watumiaji wa nyumbani.
Historia ndefu ya sera ovu
Historia inaonyesha kuwa Trump ndiye kamanda mkuu wa hivi punde zaidi wa himaya ya kibeberu ya Marekani ambayo imekuwa ikiyumba kutoka eneo moja hadi jingine tangu mwanzo wa karne ya 19.
Kulingana na data kutoka kwa shirika la World Population Review, jeshi la Merikani lilivamia kama nchi 68 kati ya mwaka 1812 na 2024.
Mara tu baada ya uhuru wa Marekani mnamo 1776, ubeberu wa Merikani umekuwa ukieneza misimamo yake katika mabara - ukipigana vita rasmi na vya wakala, ukiendesha shughuli za kuingilia wazi na za siri, na kunyakua eneo.
Historia ya uchokozi na sera za kigeni za Marekani imerekodiwa kwa kina katika kitabu cha 2014 kinachoitwa kwa njia ifaayo, ‘America Invades: How We've Invaded or Been Militarily Involved with Almost Every Country on Earth’.
Kulingana na kitabu hicho, kati ya mataifa 194 yanayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, Marekani imevamia angalau 84 kati yao na imeshiriki kijeshi na 191 - ambayo inaacha nchi tatu tu: Andorra, Bhutan, na Liechtenstein.
Tofauti na kile kilichojiri katika karne ya 19, hata historia ya hivi majuzi - baada ya Vita vya Kidunia vya pili - inakabiliwa na vita vya kikatili vya Marekani na uingiliaji ambao umesababisha ukiukwaji wa haki za binadamu, na unyakuzi wa maeneo.
Uingiliaji wa Marekani katika masuala ya nchi zingine
Haya ni mifano ya matukio machache maarufu ya sera ya kigeni ya Marekani tangu mwisho wa Vita vya Kidunia vya pili mwaka wa 1945.
Mnamo 1953, Mmerekani ilipeleka kitengo cha ujasusi (CIA) nchini Iran kuandaa mapinduzi dhidi ya serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ya Waziri Mkuu Mohammad Mossadegh.
Mnamo 1960, Marekani ilituma CIA kumuua kiongozi wa Kongo Patrice Lumumba kwa kufanya kazi na Muungani wa Usovieti. CIA yenyewe imeonyesha kwa fahari maovu yake nchini Kongo kwenye tovuti yake rasmi.
Kisha kukaja ushirikiano wenye kuleta uharibifu wa miaka 20 wa Marekani na ule uliokuwa Muungano wa Sovieti katika Vita yenye sifa mbaya ya Vietnam, kuanzia 1955 hadi 1975.
Marekani ilipanua Vita vya Vietnam kupitia uvamizi mkali wa kijeshi nchini Kambodia mnamo 1970.
Miaka mitatu baadaye, Marekani iliingilia katika nchi ya Chile ili kuunga mkono udikteta wa Augusto Pinochet mnamo 1973.
Kisha tukashuhudia utawala wa kijeshi wa Marekani ukiingilia kwa uwazi katika Vita vya Ghuba vya 1991 nchini Iraq, uvamizi wa Magharibi wa 2001 ulioongozwa na Marekani nchini Afghanistan, na baadaye kurudi kwa Vita vya Ghuba nchini Iraqi mwaka wa 2003, kupinduliwa kwa serikali ya Haiti mwaka wa 2004, kulipuliwa kwa Libya mwaka 2011, na kuingilia kati kwa Syria 2014.
Hoja nzima ya kusimulia ratiba hii mbaya ya uhasama wa sera za kigeni za Marekani ni kuelewa ukweli mmoja kuhusu siasa za kisasa za jiografia - marais hubadilika katika Ikulu ya White House, lakini sera ya mambo ya nje ya kujitanua imebaki vile vile.
Tofauti ya mienendo ya Marekani
Wakati huo, tulikuwa na milipuko ya mabomu ya Vietnam, Hiroshima-Nagasaki, Vita vya Ghuba, na Afghanistan.
Leo, ajenda ni kuhusu Gaza, Kanada, Greenland, na Panama.
Bila shaka, hatua zinazokuja huenda zisihusishe umwagaji damu. Walakini, utawala wa ubeberu utaendelea kuwinda shabaha zingine mpya.
Ni muhimu kutambua kwamba tishio la juu la Trump la kuchukua Gaza haitakuwa rahisi kwa ulimwengu kupuuza.
Hiyo ni kwa sababu Marekani, kwa muda mrefu, amekua mnyanyasaji mwenye ushawishi mkubwa zaidi ulimwenguni linapokuja suala la kambi za kijeshi za ng'ambo.
Hadi hivi majuzi, Pentagon ya Marekani iliripotiwa kuwa na angalau kambi 750 za kijeshi katika sehemu mbali mbali za ulimwengu, zikichukua karibu nchi 80.
Marekani inawekeza zaidi katika jeshi lake kuliko nchi kadhaa kwa pamoja. Kambi nyingi za Marekani ziko Japan, Ujerumani, na Korea Kusini.
Hali hii ya kudumu ya uwepo mkubwa wa kijeshi wa ng'ambo wa Marekani inasisitiza nguvu ya ubeberu wa kisasa wa Marekani.
Pia inaeleza kwa nini idara ya Trump, licha ya kutotaka kuanzisha vita vya kawaida, ina ujasiri wa kudai haki juu ya Gaza na malengo mengine mapya.
Mwanadiplomasia wa zamani wa Marekani, Henry Kissinger, aliwahi kuandika: "Mpangilio mpya wa kimataifa hauwezekani bila mchango mkubwa wa Marekani."
Kwa bahati mbaya, kwa zaidi ya miaka 200 hadi sasa, 'mchango huo muhimu wa Marekani' kwa kiasi kikubwa umekuwa wa ajabu, usio karibishwa, na usio leta furaha.
Trump na njama yake ya Gaza ni mfano mmoja tu katika mlolongo mrefu wa kile kinachoitwa michango muhimu ya Kimarekani ya Kissinger.
Kwa kusikitisha, kunaweza kuwa na mengi zaidi yajayo - wakati wa Trump na atakayekuja baada yake.
Mwandishi, Nadim Siraj, ni mwandishi wa habari kutoka India ambaye anaandika kuhusu masuala ya diplomasia, migogoro, na masuala ya kimataifa.
Maoni yaliyotolewa na mwandishi hayaakisi maoni na sera za uhariri za TRT Afrika.