Takriban vifo 42 vimerekodiwa kutokana na mlipuko wa surua katika muda wa wiki moja katika jimbo la kaskazini mashariki la Adamawa nchini Nigeria, mamlaka za afya zimethibitisha.
''Mlipuko wa surua umeathiri zaidi maeneo mawili ya serikali za mitaa ambapo vifo 42 vilirekodiwa kati ya karibu kesi 200 zinazoshukiwa,'' amesema Felix Tangwami, kamishna wa afya wa Adamawa. "Chanjo ya surua imetolewa kwa maeneo hayo na timu zetu za uwanjani zinadhibiti hali hiyo," aliyendelea kusema Tangwami katika mkutano na wanahabari.
Surua ni virusi vinavyoambukiza sana, vinavyoambukizwa kwa njia ya hewa ambavyo huathiri zaidi watoto chini ya umri wa miaka 5.
Inaweza kuzuiwa kwa dozi mbili za chanjo na zaidi ya vifo milioni 50 vimeepukwa tangu 2000, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni.
Ukosefu wa usalama ulioenea katika majimbo mengi ya kaskazini mwa Nigeria mara nyingi unalaumiwa kwa kuvuruga kampeni za chanjo, na kuwaacha watoto katika mazingira magumu zaidi.