Fulgence Kayishema alikamatwa Afrika Kusini siku ya Alhamisi kufuatia kibali cha kukamatwa kwake kilichotolewa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya Rwanda.
Amekuwa akisakwa tangu mwaka 2001.
Serikali ya Afrika Kusini inasema atafikiswha mahakamani leo Ijumaa tarehe 26 Mei katika jiji la Capetown.
"Leo ni siku ya kuwafikiria wahanga na manusura wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi. Ingawa miaka ishirini na tisa imepita, wanaendelea kubeba makovu ya kimwili na kiakili ya mateso yao," Serge Brammertz, mwendesha mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Umoja wa Mataifa amesema.
"Kukamatwa kwa Kayishema kunatoa ujumbe mzito kwamba wale wanaodaiwa kufanya uhalifu huo hawawezi kukwepa haki na hatimaye watawajibishwa, hata zaidi ya robo karne baadaye," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutterres amesema kupitia kwa msemaji wake.
Je tunajua yapi kuhusu Fulgence Kayishemi?
Fulgence Kayishema alishtakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Umoja wa Mataifa, ICTR, mwaka 2001 kwa mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa kabila la Watutsi nchini Rwanda, katika wilaya ya Kivumu, Mkoa wa Kibuye mwaka 1994.
Mahakama inadai Kayishema mweye umri wa miaka 61, alishiriki moja kwa moja katika kupanga na kutekeleza mauaji haya, ikiwa ni pamoja na kununua na kusambaza petroli ili kuchoma kanisa lenye wakimbizi ndani.
Hati ya mashtaka inadai kuwa Kayishema,afisa wa zamani wa polisi, pamoja na wahusika wengine, waliwaua zaidi ya wanaume, wanawake, wazee na watoto wakimbizi zaidi ya 2,000 katika Kanisa la Nyange katika wilaya ya Kivumu.
Fulgence Kayishema mwenye umri wa miaka 61 anadaiwa alikuwa akiishi chini ya jina la uongo kwenye shamba la zabibu wakati wa kukamatwa kwake nchini Afrika Kusini.
Wakati wa kukimbia haki, Kayishema anadaiwa alitumia majina mengi ya uwongo na kuficha utambulisho wake na uwepo wake.
Mwaka 2012, Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda, ICTR, yenye makao yake makuu nchini Tanzania iliamua kwamba akikamatwa, Kayishema atahamishiwa Rwanda kwa ajili ya kesi yake.
Tangu 2020, Timu ya Ufuatiliaji ya mahakama hii ya kimataifa imesema kumekuwa na watoro watano, wakiwemo Félicien Kabuga, Augustin Bizimana, Protais Mpiranya, na Phéneas Munyarugarama.
Sasa kuna watoro watatu wa Rwanda wanaosalia kukamatwa.
Mauaji ya kimbari nchini Rwanda yalifanyika mwaka 1994 katika siku 100 na takriban watu laki nane walipoteza maisha yao.